Jumatano, 23 Agosti 2017

Majengo na Matawi ya CCM, Yaendane na kasi ya chama


MAKAMO Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema lazima majengo na matawi ya CCM, yaendane na kasi ya chama hicho kwa kujenga majengo ya kisasa.

Alieleza kuwa wakati wa uongozi wa Chama cha ASP na TANU, wanachama na viongozi wa vyama hivyo, walijitahidi kujenga majengo, ambayo kwa sasa yamerithiwa na CCM, hivyo lazima kuwe na majengo yanayofanana na wakati uliopo.

Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alieleza hayo kwenye tawi la CCM la Pandani Jimbo la Mgogoni, kabla ya kuweka jiwe la msingi la tawi hilo, ikiwa ni sehemu ya ziara yake kiswani Pemba kwa  kuangali utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Alisema, huu ni wakati wa CCM, hivyo majengo yaliorithiwa kutokwa kwa ASP kwa Zanzibar na TANU kwa Tanzania bara kama hayaendani na kasi, ni vyema yakajengwa mengine ili yafanane na wakati na hadhi iliopo.

Alieleza kuwa, ujenzi wa tawi hilo jipya uliofanywa na wanaCCM wenyewe na viongozi wao wengine, unafaa kuungwa mkono na kila mmoja, maana wajenzi wa matawi hayo ni wanaCCM wenyewe, kama walivyofanywa waasisi wa chama hicho kutoka TANU na ASP kwa wakati wao.

“Wana wa ASP na TANU, walijenga matawi ya chama kwa njia ya kuchangishana, na leo hii tumeyarithi tukiwa na CCM, hivyo lazima na sisi tuliopo ndani ya CCM, tujenge majengo ya kisasa, ili yafanane na hadhi na ukubwa wa chama chetu”,alieleza.

Katika hatua nyengine, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar, amemshauri Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mberwa Hamad Mberwa, kuhakikishga shilingi milioni 26, zinapatikana.
Alisema kwa vile taarifa ya ujenzi inaonyesha bado shilingi milioni 36 ili kukamilisha ujenzi huo hadi kuhamia, yeye atawasilisha shilingi milioni 10, na fedha nyengine zilizobakia lazima uongozi wa mkoa uzipate kwa kuchangishana ilikulijenga tawi hilo.

Alifahamisha kuwa, kwa upande wa Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni Shehe Hamad Matari, ameshajitahidi kuchangia asilimia 75 ya gharama zilizofikiwa, hivyo ni vyema na uongozi wa Mkoa huo, kuhakikisha unazipata fedha nyengine.

“Mwenzetu Mwakilishi wa Jimbo hili la Mgogoni, ameshajitolea na sasa na wewe Mwenyekiti wa CCM Mkoa lazima shilingi ,milioni 26, zitafuteni na zangu shilingi milioni 10 zipo, wakati wowote hata leo”,alisisitiza.

Wakati huo huo, Dk Shein alizindua jengo jipya la skuli la madarasa manne ya Mgogoni, na kuwataka wanafunzi kusoma na kueleza kuwa kazi iliopo mbele yao ni kusoma na sio vyenginevyo, kwani elimu ndio msingi wa maisha yao ya baadae.

Aidha aliendelea na kauli yake, ya kuwataka waalimu kuingia madarasani na kuwasomesha wanafunzi hao, na kuweka kando siasa zao wanapokuwa madarasani. “Tumeshawawekea mazingira mazuri ya kusomesha kwa ufunguzi wa jengo jipya, sasa acheni siasa ingieni madarasani kwa wakati ili kuwapa vijana elimu”,alifafanua.

Hata hivyo, aliendelea na msimamo wake wa kumtaka Mkuu wa Mkoa kufanya ziara za mara kwa mara kwenye skuli mbali mbali, na iwapo watawabaini waalimu watoro awasiliane na Waziri husika, kwa hatua.

Aliongeza kuwa yeyote aliyekuwa hawezi kusomesha aseme kwani kuna kundi kubwa la walimu waliomaliza masomo katika vyuo vikuu vya hapa nchini na bado hawajaajiriwa. Pia, aliwasisitiza wasichanganye elimu na siasa wakati wakiwasomesha wanafunzi na kuwaeleza walimu kuwa wawasomeshe wanafunzi kama walivyosomeshwa wao.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Khadija Bakari alisema kuwa ujenzi wa madarasa hayo ulianza kwa nguvu za wananchi mnamo mwaka 2010 waliochangia TZS milioni 7.5 na baadae Serikali ikamalizia kwa kiasicha TZS milioni 64.6 na hadi kukamilika zimetumika TZS milioni 72.4. 

Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Riziki Pembe Juma, alisema kuwa anajiskia faraja kuona rais huyo, anazindua majengo mapya ya skuli, ambapo hiyo ni ishara ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Mapema Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi na Waziri asiekuwa na wizara Maalum Said Soud Said, alisema ujenzi wa masoko na skuli ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, chama ambacho ndio kilichoshinda kwenye uchaguzi mkuu.

“CCM ndio chama kilichoshinda na mimi na mwengine yoyote lazima atekeleze Ilani yake, na asietaka akae pembeni, maana uchaguzi mwengine hakuna hadi mwaka 2020”,alifafanua  Said Soud.

Nao viongozi wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Washauri wa Rais, Makatibu Wakuu nao waliwasisitiza wanafunzi kusoma kwa juhudi na Serikali yao itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwajengea majengo bora ya skuli ili kuwapa elimu bora. 

Akiwa kwenye ukaguzi wa ununuzi wa karafuu kwenye kituo cha ZSTC Bandarini Wete, Rais Dk. Shein, ameutaka uongozi wa ZSTC, kuhakikisha karafuu zilizokamatwa kutoka Mkoani Tanga, hazichanganywi na karafuu za Zanzibar. 

Aidha, aliutaka uongozi wa Mkoa wa kaskazini Pemba, kufauta taratibu za kisheria juu ya chombo aina ya jahazi kilichokamatwa hivi karibuni na karafuu zilizodaiwa kutaka kusafirishwa kimagendo.

Dk. Shein aliutaka uongozi wa Polisi katika Mkoa huo kumpa taarifa ndani ya wiki mbili juu ya hatua zilizofikiwa kwa watu waliotajwa ambao wamekimbia baada ya chombo chao kukamatwa kikiwa kinasafirisha karafuu kwa njia ya magendo. 

Rais Dk Ali Mohamed Shein, ataendelea na ziara yake ya siku tano kisiwani Pemba, kwa kumalizia Mkoa wa kusini Pemba, ambapo awali, atapokea taarifa ya kikazi ya mkoa huo, ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi.





Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar akisalimia na Mwenyeji wake Ndg. Haji Mkema mara tu baada ya kuwasili Pandani ambao Mhe. Rais ataweka jiwe la Msingi katika Tawi la CCM la Pandan












Waziri wa Fedha Dkt. Khalid akijitambulisha mbele ya wananchi, walimu na wanafuzi wa skuli ya mgogoni


















Mhe. Rais akiwasili hapo Junguni kwa ajili ya uzinduzi wa kituo kipya cha Afya ya Mama na Mtoto

Dkt. Shein akisalimiana na baadhi na watumishi na wageni mbali mbali mara tu baada ya kuwasili hapo junguni
Dkt. Shein akisalimiana na baadhi na watumishi na wageni mbali mbali mara tu baada ya kuwasili hapo junguni
Dkt. SHEIN akizindua rasmi kituo cha afya ya mama na mtoto hapo junguni




Mhe. Rais akisalimia na Viongozi mbali mbali mara tu baada ya kufika hapo Bandarini wete kwa leongo la kuangalia shughuli zaununuzi wa zao la karafuu








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni