Ijumaa, 5 Juni 2015

Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Mhe. Omar Yussuf Mzee akabidhi Vifaa kwa CCM



MJUMBE wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi Mhe. Omar Yussuf Mzee, amesisitiza haja ya kuendelea kusaidia kwa hali na mali CCM kadri hali ya kiuchumi itakavyoruhusu.

Akizungumza katika hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa vya Ofisini ikiwemo Kompyuta na Printer hapo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, amesema amelazimika kutoa msaada kwa dhamira ya kurahisisha shughuli za Kiutendaji kwa Watumishi wa CCM katika kutekeleza majukumu yao siku hadi siku.

Mjumbe huyo wa NEC ambaye pia ni Mwakilishi wa Kuteuliwa amesema kutoa ni moyo, na kuahidi kuendelea kukisaidia Chama hicho kadri ya uwezo itakavyojitokeza kwa maslahi ya Chama, wanachama na Taifa kwa ujumla.

“Ndugu Naibu Katibu Mkuu wa Chama changu (CCM) kwa upande wa Zanzibar, wahenga walisema kutoa ni moyo si utajiri. Nami nimeguswa na hilo nan do maana nikaamua kutoa Kompyuta Kumi na Mbili na Printa zake, kama msaada wangu kwa Chama, ili ziwasaidie Watendaji wetu kufanikisha shughuli zitakazoleta ushindi wa kishindo kwa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu”. Alidai Mjumbe huyo.

Akitoa neno la shukrani, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai ameelezea kufurahishwa kwake kutokana na msaada huo na kusema kuwa umeakuja katika wakati muafaka.

“Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi Zanzibar nachua nafasi hii kumpongeza Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa Mhe. Omar Yussuf  Mzee, kwa kutoa msaada huo wa kompyuta na printa zake zenye thamani ya Shsilingi za  Kitanzania milioni 21, umekuja wakati Chama kinahitaji sana vitendea kazi mithli ya hivyo na alimuakikishia mjumbe huyo kwamba vifaa hivyo vitagaiwa katika Wilaya zote kumi na mbili (12) za kichama Unguja na Pemba”. Alisisitiza Vuai.

Aidha, ametoa wito kwa wanachama wa Chama hicho kujitokeza na kuiga mfano huo, hasa wakati huu wa maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi mkuu wa dola uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, nchini kote.

Wakati huo huo, Wazee wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar wameelezea kuhuzunishwa na kusikikitishwa na taarifa za kifo cha aliyekuwa Mjumbe wa Baraza hilo marehemu Gharib Haji Mussa, kilichotokea Hospitali ya Mnazi Mmoja, usiku wa Ijumaa Juni 05, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Msaidizi wa Baraza la Wazee Ndg. Haji Machano, amesema marehemu amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mfupi na amezikwa leo Kijijini kwao Kombeni, Wilaya ya Magharibi, Unguja.

Amesema wakati wa uhai wake, marehemu alikuwa mchapa kazi hodari, asiyemajivuno, aliyeweka mbele maslahi ya Chama na mpenda watu wa rika na jinsia zote na mwenye ushirikiano mzuri na takriban jamii nzima ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla wake.

Amesema Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar, wanaungana na wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu katika kipindi hiki cha maombolezo na kuwataka kuwa na moyo wa subra kutokana na msiba wa mpendwa wao huyo.

Aidha, wanamuomba Mwenyezi Mungu Muumba Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, ailaze roho ya marehemu Gharib Haji Mussa mahali pema peponi. AMIN.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni