TAMKO LA PAMOJA LA VIONGOZI, WATENDAJI WA CHAMA CHA MAPINDUZI NA JUMUIYA
ZAKE WA MIKOA SITA YA KICHAMA YA
ZANZIBAR LA KUKUOMBA MAKAMU MWENYEKITI WA CCM NA RAIS WA ZANZIBAR MHE. DKT. ALI
MOHAMED SHEIN KUCHUKUA FOMU YA KUOMBA KUTEULIWA KUGOMBEA KITI CHA RAIS WA
ZANZIBAR KUPITIA CHAMA CHA MAPINDUZI KATIKA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2015
Kwa
niaba ya Viongozi, Watendaji wa Chama na Jumuiya zake wa Mikoa sita ya Kichama
ya Zanzibar, tunayo heshima kubwa leo
kusimama hapa kwa niaba yenu ili kuwasilisha tamko letu hili lenye nia na
madhumuni ya kumuomba kiongozi wetu mpendwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein,
kwenda kuchukua Fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya kiti cha Rais wa Zanzibar,
katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Awali
ya yote ninapenda kutumia fursa hii kumshukuru Mola wetu mtukufu mwingi wa
rehema na muumba mbingu na ardhi pamoja na vyote viliyomo, kwa kutujaalia afya
njema na kutuwezesha kukusanyika hapa leo hii kwa salama na amani.
Kwa
niaba ya wanachama wa CCM, Jumuiya
pamoja na wananchi wote wapenda amani, umoja na mshikamano wa kitaifa wa
Mikoa na Wilaya zote za Zanzibar, sisi Viongozi wa Chama, Jumuiya pamoja na
Watendaji wa CCM kutoka Mikoa sita ya
kichama ya Unguja na Pemba, leo hii tarehe 14 Juni 2015, tumekutana hapa kwenye
ukumbi wa Nyumba za Wazee Sebleni Unguja, ili kutafakari na kujenga mustakabali
wa uhai wa Chama chetu.
Kama
tunavyofahamu kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, mwaka huu wa 2015
tunakabiliwa na Uchaguzi Mkuu wa kumchagua Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe
wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Madiwani.
Huu ni uchaguzi mkuu wa tano (5) tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa hapa Tanzania hapo mwaka 1992.
Aidha,
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) tayari imeshatangaza ratiba ya uchaguzi huo
ambao utafanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Vile vile hivi karibuni CCM imetangaza ratiba ya mchakato wa uteuzi wa
mgombea wake katika uchaguzi huo pamoja na ule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania. Ratiba hiyo imeanza tarehe
3 Juni 2015 hadi tarehe 2/7/2015.
Hadi
kufikia jana tarehe 13 Juni 2015, wakati idadi ya wanachama wa CCM waliochukua
fomu za kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imefikia 32, hakuna mwanachama wa CCM hata mmoja aliyejitokeza
kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa Zanzibar, hali
ambayo inathibitisha kwamba, wana CCM wote hapa Zanzibar bado tunaridhika na
uongozi wa Mhe. Dkt. Shein. Hivyo sisi
viongozi wa CCM wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Jumuiya zetu pamoja na
wazee wetu tumeona tunao wajibu wa kukutana ili kutafakari hali hiyo na
kuipatia majibu.
Kwa
kuzingatia historia ya Chama chetu na uzito wa changamoto iliyo mbele yetu
tumeamua kukutana pahala hapa (Nyumba za Wazee Sebleni) ili kujikumbusha wajibu
wetu kama viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, walinzi na watetezi wa Mapinduzi
matukufu ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964 ambayo ndio chimbuko la majengo
haya.
Baada
ya kutafakari kwa kina na kupima kazi iliopo mbele yetu katika kusimamia
maendeleo ya wananchi, kudumisha umoja, amani, Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar pamoja na Mapinduzi yetu matukufu ya tarehe 12 Januari 1964, kwa kauli moja tumekubaliana kumuomba
kiongozi wetu mpendwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa mara nyingine tena
ajitokeze kwenda kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya Rais wa
Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi.
Kwa
hakika tunazo sababu nyingi za kumuomba afanye hivyo, lakini kwa ajili ya
kuokoa muda ninaomba nizitaje chache kwa umuhimu wake, nazo ni kama zifuatazo:-
a)
Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein bado
anakidhi vigezo na sifa zote zinazohitajika kwa mujibu wa Katiba na sharia za
uchaguzi.
b)
Katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita ameonesha uwezo mkubwa wa kuongoza nchi yetu na kusimamia kwa ufanisi
mkubwa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 – 2015.
c)
Anao uwezo mkubwa wa kuwaunganisha
Wazanzibari na kudumisha umoja, amani, na Muungano wetu wa Tanganyika na
Zanzibar.
d)
Ameiongoza Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar yenye mfumo wa umoja wa kitaifa kwa weledi mkubwa na kuwa mfano bora
wa kuigwa na Mataifa mengine duniani.
e)
Ana tabia ya upole, uadilifu, uaminifu
na unyenyekevu kwa wananchi wa rika na jinsia zote.
f)
Hana makuu wala ubaguzi wa aina
yoyote. Ni mpenda maendeleo na
mwanamapinduzi wa kweli.
g)
Ni mwenye msimamo thabiti. Katika masuala ya msingi yanayohusu nchi na
wananchi hayumbi na wala hayumbishwi.
h)
Kuanzia tarehe 17/11/2014 hadi tarehe
4/12/2014, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, alitembelea Mikoa na Wilaya zote za
Kichama hapa Zanzibar. Katika ziara hizo
alikutana na kuzungumza na viongozi wa mashina (Mabalozi) na Maskani zote za
CCM Unguja na Pemba. Kwa kupitia
mikutano hio viongozi hao ambao ni kundi kubwa la wana CCM walimuomba Dkt. Ali
Mohamed Shein, afikirie kugombea tena nafasi hii ya Rais wa Zanzibar katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kama
nilivyoeleza hapo juu, kwa hakika sababu ni nyingi inatosha tu kusema kwamba,
kwa maoni yetu Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, bado ni jembe la kujivunia na
tunaimani kubwa ya kwamba, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ataendelea
kutuvusha na hakuna mbadala wake kwa sasa.
Hivyo
kwa heshima na unyenyekevu mkubwa tunamuomba atukubalie ombi letu hili na kwa
mara nyingine tena akachukue Fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea kiti cha Rais wa
Zanzibar kupitia CCM!
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni