Alhamisi, 8 Oktoba 2020

DK.MWINYI-ASEMA ATATATUA CHANGAMOTO ZA WAWEKEZAJI

 


MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema akipata ridhaa ya kuiongoza Zanzibar, ataweka misingi imara kwa wafanyabiashara ili wafanye biashara zitakazoleta tija nchini.

Dk. Mwinyi alisema hayo alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara kusikiliza changamoto zinazowakabili ikiwa ni mwendelezo wa kampeni za mgombea huyo, mkutano uliofanyika katika hoteli ya Golden Tulip, Malindi.

Alisema sekta biashara ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza pato la taifa hivyo atahakikisha anafungua milango ili wafanyabiashara waitumie kuimarisha mifumo ya biashara.

Dk. Mwinyi alisema ni vyema kwa wafanyabiashara wa ndani kuwa tayari kuitumia milango hiyo kwa kufanya biashara kubwa ndani ya nchi na kutokaa pembeni kupoteza fursa zitakazojitokeza.

“Ninagombea nafasi hii, kwa lengo la kuwatumikia wananchi na wafanyabiashara ni sehemu muhimu ya wananchi hivyo ninawaomba mjipanga vyema tukashirikiane na kwenda sambamba na matakwa ya wanachi wetu,” alieleza Dk. Mwinyi.

Alisema ili kufikia azma hiyo, serikali atakayoiongoza itashirikiana na jumuiya za wafanyabiashara na kuangalia sheria, kanuni, masuala ya kodi na ukataji wa leseni za biashara ili kuondoa vikwazo katika shughuli za biashara na viwanda nchini.

Akizungumzia sekta ya utalii, Dk. Mwinyi alisema ataiendeleza ili kuinua kiwango cha idadi ya watalii wanaoingia nchini lakini pia kuongeza thamani na aina za utalii kama njia moja wapo ya kuongeza mapato yanayotokana na sekta hiyo.

Alisema pamoja na Zanzibar kuendelea kuwa sekta kiongozi katika kuchangia pato la taifa, bado inapaswa kutangaza vivutio ilivyonavyo zikiwemo fukwe na kwa kuwekewa mipango madhubuti itakayowavutia watalii kuongezeka.

Kwa upande wa maendeleo ya viwanda, Dk. Mwinyi alisema sekta hiyo inahitaji mapinduzi makubwa ili isaidia ustawi wa wananchi wote wakiwemo wawekezaji wazawa kuwekeza kupitia sekta hiyo.

“Sekta ya viwanda itakapoimarika, wakulima na wafanyabiashara wadogo wataweza kutumia viwanda kwa kazi tofauti ili zilete tija kwao na taifa kwa ujumla,” aliemeza Dk. Mwinyi.

Mapema Akiwazungumza katika mkutano huyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), Ally Amour, alisema serikali ya awamu ya saba imefanya mengi kwa wafanyabiashara hali ambayo imepelekea kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi.

Alisema ni vyema anapoingia madarakani kiongozi huyo kusaidia kutayarisha mazingira mazuri ya biashara ili nchi iweze kusonga mbele zaidi kimaendeleo.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, walimuomba kiongozi huyo kuzipa kipaumbele baadhi ya changamoto zilizobakia hususani kupitia sekta ya kilimo kwa kukipa kipaumbele kilimo cha umwagiliaji maji ili kuongeza uzalishaji utakaokidhi mahitaji ya ndani chakula.

Mbali na hayo walimuomba akiingia madarakani kulipatia ufumbuzi tatizo ufungaji wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni ya watu binafsi kwani imechangia kuvuruga mfumo wa maisha na biashara za baadhi nya wafanyabiashara wanaofanya shughuli hizo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni