NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ akizungumza na Waandishi wa Habari Zanzibar juu ya masuala mbali mbali yakiwemo maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe |
Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Zanzibar , Mwl. Kombo Hassan Juma, akizungumza katika Mkutano huo wa Waandishi wa Habari. |
BAADHI ya Waandishi wa Habari walioshiriki katika Mkutano huo wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’. |
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema tayari kimekamilisha taratibu zote za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe na kumpata Mgombea Mteule Ramadhan Hamza Chande atakayepeperusha bendera ya CCM kuwania nafasi ya Uwakilishi katika Uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Octoba 27, mwaka 2018.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ huko Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, amewasihi wanachama wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla kutumia vizuri fursa hiyo kwa kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kutatua kwa haraka kero zitakazojitokeza katika jimbo hilo.
Ameeleza kuwa wananchi hao wanatakiwa kuwa makini kwa kutopoteza nafasi hiyo ikizingatiwa imebaki muda wa miaka miwili kufika uchaguzi Mkuu, hivyo mwakilishi watakaye mchagua ataweza kuendeleza mageuzi ya kimaendeleo yaliyoachwa na mtangulizi wake katika jimbo hilo.
Amesema wananchi na Wana-CCM kwa ujumla wasiangalie sifa za mgombea pekee bali watathimini hata uwezo, sera, ukomavu na mipango ya maendeleo ya vyama tisa vilivyosimamisha wagombea na hatimaye kumchagua mgombea mmoja kutoka Chama chenye sifa za ziada.
Ameongeza kwa kufafanua kuwa kupitia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020, Chama Cha Mapinduzi kimetatua kwa kiwango kikubwa kero mbali mbali ndani ya Jimbo la Jang’ombe kwa kuwapekelea wananchi huduma bora za Afya, Maji Safi na Salama, elimu, umeme na kwa sasa kunaendelea ujenzi wa mitaro mikubwa itakayoondosha tatizo la kutwaama kwa maji katika Jimbo hilo.
Pia amewataka viongozi mbali mbali wa Jimbo hilo wakiwemo masheha, viongozi wa dini, wazee pamoja na vikundi mbali mbali vya kijamii kuondosha tofauti zao na badala yake kuhubiri mshikamano, Umoja na Utulivu ili Jang’ombe iwe na maendeleo endelevu.
Akizungumzia maandalizi ya Uchaguzi huo Dk. Mabodi amesema CCM imemteuwa mgombea wake Ramadhan Hamza kuwania nafasi hiyo kutokana na aliyekuwa Mwakilishi wa Chama hicho katika Jimbo hilo kutenguliwa baada ya kukabiliwa na makosa ukiukaji wa maadili ya CCM miezi kadhaa iliyopita.
Amesema CCM itatarajia kuzindua rasmi kampeni zake za kumnadi mgombea Octoba 14, mwaka 2018 ambapo mgeni rasmi atakuwa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara Ndugu Philip Mangula na zitafungwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein Octoba 25, mwaka huu.
Alisema kupitia ufunguzi huo mgombea atakabidhiwa rasmi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ili aweze kuitafsiri kwa vitendo kwa kuendeleza kwa kasi maendeleo ya Jimbo hilo yaliyofanywa na viongozi mbali mbali wa CCM waliopita.
Alisema mgombea atapata nafasi ya kunadi sera na vipaumbele vyake atakavyotakiwa kuvitekeleza kabla ya mwaka 2020, endapo wananchi wa Jimbo hili wakimuamini na kumpa dhamana ya kuwaongoza kwa kipindi cha miaka miwili.
Dk.Mabodi akizungumzia dhana ya CCM mpya na Tanzania Mpya amesema Chama Cha Mapinduzi kwa sasa kinaendelea na zoezi la uhakiki wa matumizi ya Fedha za Mifuko ya Maendeleo ya Majimbo kwa Wabunge na Wawakilishi ili kujua fedha hizo zimetumika vipi kwa kuwanufaisha wananchi.
Amesema mbali na uhakiki huo pia Tume inayofanya zoezi hilo inafuatilia utekelezaji wa ahadi za viongozi hao zimetekelezwa kwa kiwango gani pamoja na kuhakiki Serikali imetekeleza kwa kiasi gani Ilani ya Uchaguzi ya CCM sambamba na uhakiki wa mali zote za CCM katika Mikoa yote ya Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi zoezi hilo linafanyika kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji ndani ya Chama na Serikali zake ili wananchi na wanachama wa CCM kwa ujumla waendelee kunufaika na rasilimali za nchi yao.
Amewashauri wananchi wa Jimbo la Jang’ombe kujitokeza kwa wingi katika kushiriki harakati mbali mbali ya Uchaguzi huo kuanzia hatua ya kampeni hadi siku ya Uchaguzi kwa kuepuka vitendo vyote vya uvunjifu wa amani kwani zoezi hilo lipo kikatiba.
Amesema hakuna kiongozi, Chama wala kikundi cha Kijamii chenye uwezo wa kuzuia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ama chaguzi ndogo ndogo zinazoendelea nchini zisifanyike kwani mazoezi hayo yapo kwa mujibu wa sheria ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Sambamba na hayo ameweka wazi kwamba CCM inaendelea kusimamia ibara ya Tano ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017 inayoelekeza kwamba kwa kufuata misingi ya kidemokrasia ushindi wa CCM ni lazima katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Dola.
Akizungumzia zoezi la Usajili wa kuimarisha Taarifa za Vitambulisho linaloendelea katika Wilaya mbali mbali za Zanzibar hivi sasa, Dk. Mabodi amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwani zoezi hilo lina umuhimu mkubwa kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Amesisitiza kuwa zoezi hilo la uimarishaji wa taarifa za Vitambulisho kwa watu wenye sifa lina umuhimu mkubwa hasa katika mipango ya maendeleo ya nchi na taarifa mbali mbali za wananchi katika masuala ya kijamii.
Amesema Zanzibar sio nchi ya kwanza kufanya zoezi hilo bali hata nchi mbali mbali Duniani zimekuwa zikifanya zoezi hilo kwa kuwaweka wananchi wao katika mfumo rasmi wa vitambulisho wanavyovitumia katika shughuli mbali mbali za kijamii na kimaendeleo.
Ameeleza kuwa taarifa hizo zinazowekwa katika vitambulisho zinaisaidia serikali katika masuala ya sensa ya watu na makaazi, takwimu za kitaifa, hati za kusafiria, vizazi na vifo pamoja na masuala mengine yanayohusu ustawi wa Taifa.
Dk. Mabodi amezitaja Mikoa ya Kusini Unguja na Kaskazini Unguja kuwa zoezi hilo limefanyika vizuri na kwa sasa linaendelea katika Mkoa wa Mjini Magharibi na likikamilika kwa upande wa Unguja litaendelea kwa Mikoa ya Pemba.
Kupitia Mkutano huo amewataka Masheha kuhamasisha zoezi hilo lifanyike kwa ufanisi na wasiwe vikwazo vya kuwakosesha wananchi haki zao za msingi na Kikatiba.
Pamoja na hayo amevitahadharisha baadhi ya Vyama vya Siasa kuacha tabia ya kuwapotosha wananchi na kuwazuia wasishiriki katika zoezi hilo kwani lipo kisheria na hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amekuwa akisisitiza lifanyike kwa ufanisi.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Zanzibar , Mwl. Kombo Hassan Juma, amesema suala la Uchaguzi ni mchakato wa Kidemokrasia hivyo kila mwananchi aliyetimiza umri kisheria anatakiwa kutumia haki yake ya kuchagua na kuchaguziliwa hivyo wananchi wa Jang'ombe wahamasishane kujitokeza kwa wingi kushirriki katika uchaguzi huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni