MSHINDI wa Uwakilishi tiketi ya CCM Uchaguzi Mdogo wa Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande.
MGOMBEA Uwakilishi katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la
Jang'ombe Zanzibar kupitia Chama cha
Mapinduzi Ndg Ramadhan Hamza Chande
ameibuka mshinda katika uchaguzi huo kwa ushindi wa Kura 6,581 sawa na
asilimia 90.5 ya kura zote halali zilizopigwa ambazo ni 7,274.
Akitangaza matokeo hayo
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo hilo ambaye pia ni Afisa wa Tume ya
Uchaguzi Wilaya ya Mjini Unguja, Mwanapili Khamis Mohamed amesema kufuatia
matokeo hayo Ramadhan Hamza ameshinda Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Jimbo
la Jang'ombe.
Afisa huyo amemtangaza mshindi wa pili kuwa ni Mgombea wa
Chama Cha CUF ndugu Mtumwa Ambari Abdalla aliyepata kura 172 sawa na asilimia
2.4.
Aidha ametaja kura za vyama vingine vilivyoshiriki katika
mchakato huo wa Uchaguzi ambazo ni ADA-TADEA 131, AFP 58, CCK 72, DP 73, TLP
71, SAU 53 pamoja na NRA 62.
Akizungumza mara baada ya matokeo hayo Mwakilishi wa Mgombea
wa chama cha ADA-TADEA Halma Abdalla amesema Uchaguzi huo ulikuwa huru na wa
haki hivyo mgombea wa CCM ameshinda kihalali.
Naye Mshindi wa Kiti cha Uwakilishi tiketi ya CCM Jimbo la Jang'ombe
ndugu Ramadhan Hamza Chande amewashukuru wananchi wote waliojitokeza kupiga
kura hasa wale waliomwamini na kumpa ridhaa ya kuwa Mwakilishi wa kuliongoza
Jimbo hilo.
Ameahidi kutekeleza vipaumbele vyake alivyoahidi kupitia
katika mikutano mbali mbali ya kampeni za Uchaguzi kwa mujibu wa maelekezo
yaliyomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Uchaguzi huo uliofanyika leo Octoba 27, mwaka 2018 umefanyika
kutokana na aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo ndugu Abdalla Diwani kuvuliwa
uanachama kwa makosa ya ukiukaji wa maadili ndani ya taasisi hiyo.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni