NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
ZOEZI la Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe wa kumchagua
Mwakilishi wa Jimbo hilo unaendelea vizuri bila ya kuwepo na matukio ya vurugu
na uvunjifu wa amani katika vituo vya kupigia kura.
Akizungumza Msimamizi
Mkuu wa Uchaguzi Jimbo hilo ambaye pia ni Afisa wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya
Mjini Unguja, Mwanapili Khamis Mohamed, amedhibitisha kuwa zoezi hilo
linaendelea vizuri.
Amesema wananchi wamejitokeza toka saa 1:30 asubuhi walikuwa
tayari washafika katika vituo vya kupiga kura na vituo vilipofunguliwa wamepiga
kura kwa utulivu na bado wanaendelea kujitokeza.
Afisa huyo wa Tume ya Uchaguzi Wilaya ya Mjini, amewasihi
wananchi wenye sifa za kupiga kura kisheria kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa
lengo la kutekeleza haki yao ya Kidemokrasia.
Aidha amesema mpaka hivi sasa bado hapajatokea changamoto
yoyote kwani Tume hiyo imejipanga vizuri hasa katika suala zima la kuweka
mazingira rafiki ya upatikanaji wa vifaa
pamoja na huduma za msingi za maafisa na wadau mbali mbali walioshiriki katika
kufanikisha zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa kutembelea Vituo vya kupigia kura Mgombea Uwakilishi wa Tiketi ya CCM wa Jimbo
la Jang’ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande, ameelezea kuridhishwa kwake na hali
ya utulivu katika Vituo vya kupigia kura.
Amewasisitiza wananchi wa Jimbo hilo bila ya kujali tofauti
zao za kisiasa wajitokeze kwa wingi kuchagua
mgombea watakayeona ana sifa na vigezo vya kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya Uwakilishi wa Chama cha
ADA-TADEA, Sabry Ramadhan Mzee ‘China’ , amewataka wananchi wa Jimbo la Jang’ombe
kuendeleza utamaduni wa ustaarabu na utulivu wakati wote wa zoezi hilo la
Uchaguzi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi RC-Ayoub Mohamed
Mahmoud, amesema Vyombo vya Ulinzi vimejipanga vizuri kukabiliana na changamoto
yoyote inayohusu masuala ya ulinzi na usalama ndani ya Jimbo hilo.
Amewasihi wananchi wakimaliza kupiga kura warudi majumbani
kwa lengo la kuendendelea na shughuli zao za kujitafutia kipato huku
wakisikiliza vyombo vya habari kwa ajili ya kupata matokeo ya Uchaguzi huo.
Uchaguzi huo unaofanyika leo Octoba 27, mwaka 2018 unafanyika
kwa lengo la kumpata Mgombea Uwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe kufuatilia
aliyekuwa kiongozi wa nafasi hiyo kuvuliwa uanachama na CCM kutokana na kukiuka
maadili ya taasisi hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni