MWAKILISHI wa Jimbo la Bububu Ndugu Masoud Abrahman Masoud akizungumza mbele ya wananchi hao. |
BAADHI ya wananchi hao wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab Soud. |
Shamba la Dole kwa Shabuta lenye ukubwa wa hekta 168 ambalo lina mgogoro kati ya wananchi na bi.Shafika Hamed Abdulla. |
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab Soud amewataka wananchi wanaofanya shughuli za
kilimo katika shamba lililopo Dole kwa Shabuta kuendelea kuwa wavumilivu
wakisubiri maamuzi ya Vyombo vya kisheria kutatua mgogoro wa shamba hilo.
Rai hiyo ameitoa leo wakati
alipotembelea shamba hilo lililopo Dole kwa Marehemu Mzee Shabuta lenye hekta zaidi ya 168 ambalo lina mgogoro
baina ya wananchi wanaotumia eneo hilo kwa ajili ya shughuli za kilimo na Bi.
Shafika Hamed Abdallah anayedaiwa kuwa mmiliki wa eneo hilo.
Alisema mgogoro huo tayari upo katika
ngazi ya Mahakama ni vyema wananchi hao wakaendelea kutulia huku wakifanya
shughuli zao za kujitafutia kipato mpaka mahakama itakapofanya maamuzi ya
kisheria juu ya shauri hilo.
Mwenyekiti huyo ndugu Rajab aliyefuatana na
Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharib kwa lengo la kusikiliza malalamiko ya
wananchi hao, na kusema kuwa CCM itafuatilia kwa kina ili kutatua mgogoro huo kwa njia ya amani bila
kutokea athari yoyote ya uvunjifu wa Sheria.
Alisema baada ya ziara hiyo atakaa na
Kamati ya Siasa ya Mkoa huo pamoja na viongozi mbali mbali wa serikali kwa lengo
la kujadiliana na kufikia maamuzi yatakayosaidia kusuluhisha mgogoro huo.
“Tumekutana na nyinyi wananchi na
kusikia malalamiko yenu na tunaahidi kuyafanyika kazi lakini kwa kuwa jambo
hili tayari lipo katika ngazi ya mahakama tutafuatilia kujua wapi limekwama ili
tukwamue”.amesema Mwenyekiti huyo wa CCM.
Akizungumza Mwakilishi wa Jimbo la
Bububu Masoud Abrahman Masoud, amesema ziara hiyo imefanyika baada ya wananchi
hao kumuomba wakutane na uongozi wa CCM ngazi ya Mkoa ili wawasilishe
malalamiko yao ya kuzuiliwa kufanya shughuli za kilimo katika shamba hilo wanalolitumia
kwa miaka mingi kwa ajili ya kilimo.
Mwakilishi huyo Masoud, ameongeza kuwa
kutokana na mgogoro huo kuwa wa muda mrefu huku pakizuka vurugu za mara kwa
mara kuna umuhimu wa Serikali hasa taasisi zinazohusika na utatuzi wa migogoro
ya ardhi kutafuta ufumbuzi wa haraka juu ya tatizo hilo.
Shamba hilo lenye ukubwa wa jumla ya
hekta 168 linatumiwa kwa shughuli za kilimo na zaidi ya wananchi 200 wa vijiji
mbali mbali vya Jimbo la Bububu hasa
kijiji cha Dole na vjijiji vya majimbo jirani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni