BAADHI ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Kada wa CCM Julius
Mtatiro katika Mkutano uliofanyika katika Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Julius Mtatiro amesema viongozi
mbali mbali wanahama katika Vyama vya
upinzani kutokana na taasisi hizo kushindwa kuwatumikia wananchi na badala yake
ajenda zao zinatekelezwa na CCM.
Amesema mifumo imara ya kisiasa, kidemokrasia,uwazi,
uwajibikaji, utendaji na utawala bora
iliyopo ndani ya CCM na Serikali zake mbili ya Zanzibar na Jamhuri ya muungano ndio chanzo cha wanachama
na viongozi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza na waandishi wa
Habari huko Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui, aliwambia wanachama mbali
mbali wa vyama vya upinzani hasa CUF na CHADEMA kujiunga na CCM mapema ili
wanufaike na demokrasia pamoja na siasa zenye sera halisi za maendeleo.
Kupitia mkutano huo, Mtatiro aliyewahi kushika nyadhifa za ngazi
za juu ndani ya CUF na kwa sasa amehamia CCM, alisema amepoteza miaka 10 akiwa kiongozi ndani ya CUF na UKAWA ambapo
hana jambo lolote analoweza kujivunia zaidi ya kuwa muhanga wa kutatua migogoro ndani ya taasisi hizo
iliyotokana na uchu wa madaraka.
Ameeleza kwamba licha ya vyama vya upinzani kuwa mstari wa
mbele kukosoa na kubeza kila jambo linalofanywa na Serikali lakini ukweli na
kwamba ndani ya vyama hivyo kuna mifumo ya rushwa, ufisadi, ukandamizaji wa
demokrasia, pamoja na ukiukaji wa haki za binadamu.
Akijibu baadhi ya hoja za waandishi wa habari , Mtatiro
amesema kila mtu ana haki ya kuhama chama kimoja kwenda kingine na yeye
amefanya hivyo baada ya kuvutiwa na mfumo imara wa kisiasa ndani ya CCM chini ya Mwenyekiti wa Chama
hicho Dkt. John Pombe Magufuli.
“ Kama niliweza kukaa ndani ya CUF miaka 10, basi hata CCM
Mwenyezi Mungu akinipa uzima nitakaa zaidi ya miaka 60 kwani Chama hiki
kimetekeleza mambo mengi mazuri kwa muda mfupi ambayo nilitamani yafanyike kwa
Taifa letu”, alisema Mtatiro.
Amesema kuwa atabaki kuwa mwanasiasa mwenye msimamo na
asiyeyumba katika kueleza ukweli na kuonyesha njia ya mafanikio kwa wananchi
wenzake.
Akizungumzia hali ya maisha ya wananchi hasa wa Vijijini
amesema yameimarika kwani huduma muhimu za kijamii na kiuchumi zimeboreshwa
hasa Barabara Afya , Elimu , Umeme, Maji safi na salama.
Pia akizungumzia Sera ya Tanzania ya Viwanda Mtatiro, amesema mkakati huo ndio chimbuko la kukuza kwa kasi uchumi wa Taifa na kuongeza kuwa
sera hiyo inatakiwa kwenda sambamba na kampeni uzalishaji mkubwa wa malighafi
kupitia Sekta ya Kilimo.
Amesema Mataifa yaliyoendelea yamewekeza zaidi katika ujuzi
na ufundi hasa kwa kundi la vijana ambalo ndio nguvu kazi ya uzalishaji katika
Sekta mbali mbali za umma na binafsi.
Katika maelezo yake mtatiro, ameshauri CCM kupitia Serikali
zake kuaulisha changamoto za ajira kwa vijana kupitia mfumo wa kujenga Vyuo
vingi vya Ufundi na Ujasiriamali ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa
kutengeneza bidhaa mbali mbali zitakazochangia kwa kiwango kikubwa katika
ukuaji wa uchumi wa Taifa.
“ Nazishauri Serikali zetu badala ya kutumia fedha nyingi kuwasomesha vijana
Vyuo Vikuu pia waangazie katika ujenzi wa Vyuo vya Ufundi na Ujasiriamali kila
Kata na Shehia ili tupate vijana wengi wenye ujuzi ambao wataweza pia kujiajiri
wenyewe kwani mataifa mengi yaliyoendelea kiuchumi kama China,Marekani na India wametumia mfumo huo na wameweza kufika mbali kiuchumi.”, ameshaSEuri Mtatiro.
Mwanasiasa huyo ambaye pia ni mchambuzi, mtafiti na mwandishi
wa makala mbali mbali za Kisiasa nchini amezungumza na Vyombo vya Habari vya Zanzibar kwa mara ya kwanza toka alipohama
CUF na kujiunga na CCM mnamo Desema 11,
mwaka 2018.
|
Big up Mtatiro, ulipotea tu
JibuFuta