Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ndugu Salum Kassim Ali (kulia) akisalimiana na Mwakilishi mteule wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande(kushoto) mara baada ya hafla ya kukabidhiwa Cheti cha udhibitisho wa ushindi.
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MWAKILISHI mteule wa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Jimbo la Jang'ombe Ndugu Ramadhan Hamza Chande leo amekabidhiwa rasmi Cheti cha udhibitisho wa ushindi wa nafasi ya Uwakilishi wa Jimbo hilo.
Hafla hiyo imefanyika katika Ofisi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Wilaya ya Mjini iliyopo Maisara na kuudhuriwa na Viongozi na Wanatendaji wandamizi Tume hiyo na CCM.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Cheti hicho Mwakilishi mteule huyo Ramadhan Hamza ameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kwa kufuata miongozo na taratibu zote za kisheria kwa maslahi ya wananchi wote wa Jimbo hilo.
Amewashukuru wananchi na wanachama wa CCM wa Jimbo hilo kwa kumpatia ridhaa ya kuongoza Jimbo hilo kupitia utaratibu halali wa kidemokrasia.
"Nitawatumikia kwa uadilifu wananchi wote wa Jang’ombe bila ya ubaguzi wowote kwani naamini bila nyinyi kuridhia na kunichagua kwa kura nyingi nisingeweza kushinda katika mchakato huu wa kisiasa uliokuwa na ushindani mkubwa.
Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 tayari nishakabidhiwa muda wowote nitaanza kutekeleza mpango kazi wangu kwa lengo la kutekeleza ahadi nilizoahidi katika kampeni.”,ameeleza Chande.
Kwa upande wake aliyekuwa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Jang'ombe ambaye pia ni Afisa wa ZEC Wilaya ya Mjini Bi.Mwanapili Khamis Mohamed amemsisitiza kiongozi huyo kufanya kazi zake kwa majibu wa taratibu na kanuni za kisheria ili kutimiza matakwa ya wananchi waliomchagua.
Mwakilishi huyo aliyeshinda nafasi hiyo jana kwa kura 6,581 sawa na asilimia 90.5 katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang'ombe uliofanyika kwa amani bila ya kujitokeza matukio ya uvunjifu wa sheria za Uchaguzi na nchi kwa ujumla.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni