NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) ndugu Humphrey Polepole amesema njia pekee ya CCM kulipa wema kwa wananchi ni viongozi wake kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuleta maendeleo endelevu nchini.
Amesema wananchi wamekiamini Chama na kukipa ridhaa ya kuongoza Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutokana na usimamizi na utekelezaji mzuri wa Sera zake kwa jamii.
Rai hiyo ameitoa leo katika hafla ya kukabidhi mipira ya kusambazia maji safi na salama kwa wananchi wa Jimbo la Tunguu huko katika ukumbi wa T.C uliopo Dunga Wilaya ya Kati Unguja.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi mipira hiyo kwa uongozi wa Jimbo la Tunguu kwa niaba ya wananchi, Ndugu Polepole amesifu juhudi za kuwatumikia wananchi zinazofanywa na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo hilo.
Polepole amewataja viongozi hao ambao ni Mbunge wa Jimbo hilo Khalifa Salum Said na Mwakilishi wa Jimbo hilo Simai Mohamed Said kuwa wametoa mipira hiyo kwa lengo la kumaliza changamoto ya ukosefu wa huduma za maji.
Ndugu Polepole alisema Viongozi wa Chama na Serikali hasa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani nchini wanatakiwa kuendeleza utamaduni wa kufanya kazi na kuwapelekea wananchi maendeleo na sio ahadi za uongo.
Katibu huyo wa NEC,Polepole amefafanua kuwa maisha ya mwanadamu yeyote yanahitaji maji hivyo Kitendo cha kuwapelekea wananchi huduma hiyo ni kuharakisha maendeleo ya jimbo kwani wananchi watafanya shughuli za kujiingizia kipato kwa utulivu.
Kupitia hafla hiyo, kiongozi huyo amewataka viongozi wa majimbo mengine Zanzibar kuiga mfano huo wa kutatua kero za wananchi ili ifikapo mwaka 2020 CCM iwe imetekeleza ahadi zote zilizotolewa katika Uchaguzi Mkuu wa Dola uliopita.
Katika maelezo yake Polepole,ametangaza rasmi kuwa kiongozi yeyote atakayeshindwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 asitarajie kupewa tena nafasi ya uongozi kupitia Chama Cha Mapinduzi kwani anakuwa haitoshi kiutendaji.
Pia amesema suala la Serikali kufanya kazi kwa pamoja na Chama sio jambo la hiari bali ni lazima linalotakiwa kufuatwa na viongozi wa mamlaka hizo.
Polepole ameeleza kuwa CCM inaendeleza kuwa na mvuto kwa wananchi na mataifa mengine Duniani kutokana na kutawaliwa na dhana ya ukweli na uwajibikaji katika kutekeleza Sera zake.
Polepole ameziagiza Halmashauri zote za Wilaya Zanzibar kuhakikisha zinatenga fedha ya mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake na vijana ili wajikwamue kiuchumi na kunufaika na matunda ya nchi yao.
"Wanawake na Vijana ni miongoni mwa walipa kodi hivyo kupewa mikopo ni moja ya fursa yanayostahiki kupata kwa lengo la kujikwamua kiuchumi",amesema Polepole na kuongeza kuwa kila mwananchi ana haki ya kunufaika na matunda ya Zanzibar.
Sambamba na hayo amesisitiza suala la maadili kwa viongozi, watendaji na wanachama wote wa CCM kwa lengo la kuendeleza misingi na Itikadi bora za kisasa ndani ya CCM.
Pamoja na hayo ametoa tahadhari kwa viongozi na wanachama wanaendeleza kampeni za kuwania Kiti cha Urais wa Zanzibar kuacha tabia hizo kwani bado nafasi hiyo ina mwenyewe ambaye ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Akizungumzia namna CCM ilivyoimarika alisema taasisi hiyo inashinda kwa kishindo katika Chaguzi ndogo ndogo za Kata na Majimbo ya Tanzania bara, hatua inayoimarisha CCM na kudhoofisha upinzani.
Aliwapongeza Marais wote akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutekeleza ipasavyo Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo la Tungu ndugu Simai Mohamed Said,amesema ataendelea kuimarisha huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi ndani na maeneo jirani ya Jimbo hilo.
Alisema anashirikiana vizuri na viongozi wengine wa Jimbo hilo ambao ni Mbunge, Madiwani na viongozi wa Kamati ya Siasa ya Jimbo kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi mbali mbali ya maendeleo.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo ndugu Khalifa Salum Said, amesema viongozi hao wamejipanga kumaliza kero ya upungufu wa maji safi na salama katika Vijiji mbali mbali vilivyomo katika Jimbo la Tunguu.
Mipira hiyo ya Maji Safi na Salama imegharimu kiasi cha shilingi milioni tano ambayo ni awamu ya tatu ya usambazaji wa miundombinu ya maji katika Jimbo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni