Jumanne, 27 Novemba 2018

DK.MABODI AENDELEA NA ZIARA YAKE HALMASHAURI YA WILAYA YA KATI UNGUJA.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


 NAIBU KATIBU MKUU WA CCM ZANZIBAR DK.ABDULLA JUMA  SAADALLA AKIKAGUA MASHINE YA KUTENGENEA MAZIWA KATIKA KIKUNDI CHA WAJASRIAMALI CHA MPAPA WILAYA YA KATI UNGUJA KATIKA ZIARA YAKE.

 CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) kimesema kitaendelea kufuatilia na kusimamia kwa  karibu utendaji wa Serikali za Mitaa ili zilete maendeleo endelevu kwa jamii. 
Ufafanuzi huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi ameutoa leo katika mwendelezo wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Kati Unguja, ameeleza kwamba Sera za CCM zimejielekeza katika kutatua kwa vitendo changamoto zinazowakabili wananchi wa Mijini na Vijiji. 
Amesema lengo la Serikali Kuu kupeleka madaraka ngazi za Serikali za mitaa kupitia mfumo wa ugatuzi imelenga kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kijamii na zenye viwango.
Dk. Mabodi amewambia Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali kuwa wanatakiwa kutumia muda mwingi katika maeneo mbali mbali ya Kijamii kwa dhamira ya kuratibu na kutafuta njia bora za kutatua kero za wananchi.
Katika maelezo yake, Dk.Mabodi ameeleza kwamba CCM inafuata falsafa ya Uongozi Shirikishi na Jumuishi kwa lengo la kuzisimamia Serikali zitekeleze kwa ufanisi Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020.
Naibu Katibu Mkuu huyo,  Dk. Mabodi amesema CCM haina muda wa kufanya siasa za marumbano,mihemuko na machafuko bali viongozi wake wanakesha usiku kucha wakibuni njia bora za kuzisimamia Serikali zake zifanye Mapinduzi ya kihistoria katika Nyanja za Kiuchumi, Kijamii ,Kisiasa na Kimaendeleo. 
Pia ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kati kwa hatua kubwa waliyopiga katika kutekeleza miradi katika Sekta za Elimu, Kilimo Afya pamoja na ukusanyaji wa mapato kupitia mpango wa ugatuzi. 
Aidha amewataka wananchi maendeleo kuendelea kuamini na kuthamini, juhudi zinazofanywa na viongozi wakuu wa Serikali ambao ni Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa maarifa na uadilifu wa kuweka mazingira salama ya ulinzi wa rasilimali za nchi huku wakidhibiti rushwa,ufisadi na matumizi mabaya ya mali za umma. 
Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu wa CCM DK. Mabodi ametoa ahadi ya kuchangia shilingi milioni Moja kwa maskani ya CCM ya Kijibwe Mtu pamoja na kuchangia fedha za matengenezo ya Choo cha Skuli ya Maandalizi ya Kijiji hicho cha Kijibwe Mtu sambamba  kuchangia masuala mbali mbali ya miundombinu ya kijamii katika Wilaya hiyo ya Kati Unguja. 
Pamoja na hayo DK. Mabodi amempongeza Diwani wa Wadi ya Chwaka,Mlenge Hatib Mlenge kwa juhudi zake za kusimamia vizuri miradi  ya ujenzi wa miundombinu ya Skuli ya Msingi Chwaka pamoja na Skuli ya maandalizi ya 'Kiu' itakayohudumia wanafunzi wa Vijiji vya Kijundu na Uchuchuma.
Akizungumza Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Said Mtaji Askari amesema Halmashauri imekuwa ikitekeleza miradi mbali mbali ambayo ni  vipaumbele muhimu kwa jamii.
Alitoa Taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kati Unguja ya utekelezaji wa Ilani ya CCM,Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mohamed Salum Mohamed  amesema makisio ya makusanyo ya fedha kwa mwaka 2018/2019 ni shilingi 800,000,000 kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Novemba mwaka 2018 wamekusanya shilingi 236,215,050 kutoka katika vyanzo tofauti vya mapato sawa na asilimia 29.
Amesema wamehamasisha wananchi kuunda vikundi vya ushirika vya uzalishaji mali na kuweka na kukopa sambamba na kukuvisajili vikundi 60.
Kwa upande wa fedha za mfuko wa maendeleo ya jimbo zinazoingia katika Halmashauri hiyo   wametoa vifaa vya ujenzi katika skuli Tisa za maandalizi na kutoa vifaa vya kusambazia maji katika shehia nane. 
Aidha amesema wameongeza idadi ya mabibi shamba na mabwana shamba pamoja na kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wakulima, pamoja na kuongeza idadi ya uzalishaji wa mpunga kutoka  0.7 hadi 1.6.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo, amezitaja changamoto zinazowakabili Halmashauri hiyo kuwa ni ukosefu wa maabara za Sayansi katika skuli mbali za Sekondari hali inayochangia wanafunzi wengi kutofaulu masomo ya Sayansi. 
Aidha ameitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa madawati kwa skuli za maandalizi, msingi na Sekondari. 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe.Mashavu Sikwa akijibu hoja za baadhi ya washiriki katika ziara hiyo juu ya uwepo wa vitendo vya wizi wa mazao na Mifugo kwa baadhi ya maeneo,amesema njia pekee ya kudhibiti vitendo hivyo ni wananchi kushirikiana katika kufanya ulinzi shirikishi wa Polisi jamii. 
Akizungumzia  changamoto zinazowakabili wananchi wa Shehia ya Kijibwe Mtu, Diwani wa Wadi ya Bambi Rashid Abass Othman amesema wana ukosefu wa huduma ya umeme, maji safi na salama pamoja na huduma za Afya kuzifuata masafa ya mbali na Kijiji hicho. 
Mwenyekiti wa Wilaya ya Kati Unguja,Hassan Mrisho Vuai amewataka watendaji wa Halmashauri kuwa wabunifu zaidi katika kuitumikia jamii. 
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Mabodi amekagua miradi mbali mbali ikiwemo Vyuo Dunga Kiembeni, Skuli ya Maandalizi Chwaka, Ujenzi wa Skuli ya Kijundu, Utiaji wa umeme Skuli ya Jumbi,Ujenzi wa Choo Skuli ya Kikungwi pamoja na kutembelea Skuli ya maandalizi Kikungwi.
Miradi nyingine ni Skuli ya maandalizi Umbuji, Utiaji wa umeme kisima cha jamii Mitakawani, mradi wa kusanifu maziwa ya Ng'ombe na Mbuzi Mpapa pamoja na mradi wa umeme wa Nguvu za Jua kisima cha Maji cha Kijibwe Mtu. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni