Jumatano, 28 Novemba 2018

DK.MABODI AENDELEA NA ZIARA YAKE MANISPAA YA MAGHARIB 'A', AWAONYA WANAOBEZA JUHUDI ZA SMZ.


 NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi akikagua utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Manispaa ya Magharibi 'A'   katika Skuli ya Msingi ya Kihinani.

 
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi (wa kwanza kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharib Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud na viongozi na watendaji wa Manispaa ya Magharib 'A'  wakikagua mashine ya kukausha dagaa inayomilikiwa na Kikundi cha ujasiriamali cha 'TUSIYUMBISHANE' kinachonufaika na fursa za ugatuzi.
 
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi  akikagua Kituo cha Afya cha Bumbwisudi kilichojengwa na wadau wa maendeleo wa Milele Foundation ambayo kipo katika Mfumo wa Ugatuzi.


 Daktari Dhamana wa Kituo cha Afya cha Bumbwisudi Said Fadhil Abbass, akieleza maendeleo yaliyofikiwa katika kituo hicho cha Afya Bumbwi sudi.
  
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi  akizungumza na watendaji na viongozi wa Baraza la Manispaa Magharib 'A'  kabla ya kutembelea miradi ya maendeleo. 

Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa hiyo, Ndugu Amour Ali Mussa akisoma taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Baraza la Manispaa hiyo. 

 BAADHI ya watendani, viongozi wa Manispaa pamoja ,Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Magharib pamoja na Mkoa wa Mjini Magharib wakifuatilia maelekezo ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Dk.Abdulla Juma Mabodi.

 MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar  Ndugu Amini Salmin Amour akichangia masuala mbali mbali ya uimarishaji wa Kiutendaji katika Manispaa ya Magharib 'A'


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla 'Mabodi', amesema CCM inasimamia Sera zake ipasavyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii na kiuchumi.

Kauli hiyo ameitoa leo katika mwendelezo wa ziara yake kwa siku ya tatu ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM Katika Baraza la Manispaa ya Magharibi 'A' Zanzibar.

Amesema CCM inaamini kwamba suala la maendeleo kwa jamii halina itikadi za kisiasa bali linatakiwa kutekelezwa kwa wananchi wote bila ya ubaguzi, hatua ambayo imefikiwa kwa kiasi kikubwa na mfumo wa ugatuzi wa madaraka katika Serikali za Mitaa.

Ameeleza kwamba fikra na dhana ya zanzibar kuwa 'Singapore' ya Bara la Afrika inaendelea kutekelezwa kwa vitendo na Serikali ya Mapinduzi ya  Zanzibar inayoongozwa na CCM kupitia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Amesema sifa kuu ya viongozi wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi ni uadilifu, hekima, busara, ukweli, utu na uongozi bora katika kutatua kero za wananchi.

Kupitia ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo, Dk. Mabodi amewaonya baadhi ya wanasiasa wa vyama vya upinzani nchini kuacha tabia ya kupotosha umma kwa makusudi juu ya hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa na Serikali katika Sekta ya Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia na kueleza kuwa Sera hiyo ipo katika Ilani ya CCM na inaendelea kutekelezwa kwa kufuata matakwa ya kisheria.

" Kuna baadhi ya watu wanaojiita wanasiasa hapa Zanzibar wao kazi yao kubwa ni kuisubiri Serikali itekeleze jambo lolote la maendeleo, na wao waibuke na kukosoa na kubeza bila ya hoja za msingi ili waweze kupata siku za kuishi kisiasa.

Kwa hali hiyo nawambia kwamba hakuna wa kuzuia kasi ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo tutaendelea kufanya mambo mbali mbali tunayoyaona yana tija kwa maslahi mapana kwa wananchi kwani CCM ndio Chama tawala tulioaminiwa na wananchi wakatupa ridhaa ya kuongoza dola.", amesema Dk.Mabodi.

Dk. Mabodi amesema CCM haina mzaha wala haiwezi kuyumbishwa na wanasiasa waliochoka na kufilisika kifikra na kisiasa, bali itaendelea kuwa imara na kutekeleza kwa kasi maendeleo ya wananchi.

Naibu Katibu Mkuu huyo, amesema kwa sasa wananchi wa maeneo mbali mbali hasa waliopo pembe zoni 'Vijijini' wananufaika sana na miradi mbali mbali ya kujikwamua kiuchumi kupitia mfumo wa ugatuzi hasa katika sekta za ufugaji,kilimo,uvuvi,afya,elimu na ujasiliamali.

Pamoja na hayo Dk. Mabodi ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa Ilani ya CCM uliofanywa na Manispaa hiyo kupitia mfumo wa ugatuzi kwani umesaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi.

Akizungumza Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud ameeleza kwamba kupitia mfumo huo wa ugatuzi wataimarisha huduma bora za kijamii na kupunguza hatua kwa hatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi.

RC Ayoub ameweka bayana kuwa wananchi wanatakiwa kuendelea kutoa ushirikiano wa kudumu katika kulinda na kutumia vizuri miradi mbali mbali inayotekelezwa na ugatuzi ili iwe endelevu katika kuwasaidia wananchi wengi kwa mujibu wa mahitaji yao ya msingi.

Naye Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa hiyo, Ndugu Amour Ali Mussa amesema Baraza hilo lililenga kukusanya shilingi bilioni 1,322,381,262 hadi kufikia Septemba 2018 na limefanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 1,510,357,388 sawa na asilimia 114 ambapo wamevuka malengo 
yaliyokusudiwa.

Amesema wameendelea kupiga hatua kubwa katika Sekta zilizogatuliwa zikiwemo elimu, Afya na kilimo ambapo wananchi wa shehia mbali mbali zilizomo katika Baraza hilo wamenufaika na fursa zilizomo katika mfumo wa ugatuzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya watendaji  wanaohudumu katika mfumo wa ugatuzi ndani ya manispaa hiyo, pamoja na wananchi wanaonufaika na fursa zinazotokana na ugatuzi wamekiri kuwa utaratibu huo umeharakisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii.

Alizungumza Daktari Dhamana wa Kituo cha Afya cha Bumbwisudi Said Fadhil Abbass, amesema toka kuanzishwa kwa mfumo huo huduma za Afya zimeimarika sambamba na upatikanaji wa dawa ni kwa asilimia 99 na asilimia moja inayobaki dawa zinanunuliwa na Manispaa ya Magharibi 'A'.

Ameitaja changamoto wanayokabiliana nayo ni upungufu wa wafanyakazi kwani wananchi wanaohitaji huduma wanakuwa wengi huku wafanyakazi wakiwa ni kidogo.

Naye Afisa Mifugo wa Wilaya Magharibi 'A', Ahmada Ramadhan Nassor amesema wametoa mafunzo ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji mbali mbali pamoja na kujenga kituo cha kisasa kitakachotumika katika matibabu mbali mbali ya mifugo.

Kwa upande wake Afisa Uvuvi Wilaya ya Magharib 'A' Khamis Bai amesema katika hatua za kuwawezesha wananchi ambao ni wajasiriamali wa biashara za kukausha na kuuza dagaa katika eneo la Bububu Kihinani wanaendelea kuwekewa mazingira rafiki ya kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Amesema kwa sasa wanatumia mashine ya kisasa ya kukaushia dagaa yenye thamani ya shilingi milioni 40 inayokausha ndoo tatu zenye kilo sitini kwa masaa matatu, ambapo bado wana mahitaji ya mashine nyingine kubwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Akizungumza Kaimu Mwalimu Mkuu wa skuli ya maandalizi ya Kihinani, Mwajuma Makame Issa amesema mfumo wa ugatuzi umesaidia kuimarisha miundombinu ya utoaji wa elimu, kwani kwa sasa wanapata kwa haraka vifaa mbali mbali vya kufundishia tofauti na utaratibu uliokuwepo zamani.

Ameitaja changamoto iliyopo katika Skuli hiyo kuwa ni wingi wa wanafunzi unaosababisha vyumba vya madarasa kuwa kidogo, ambapo darasa moja linachukuwa wastani wa wanafunzi 100 kiwango ambacho ni kikubwa.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni