Jumatatu, 26 Novemba 2018

DK,MABODI AWAONYA WATENDAJI NA VIONGOZI WANAOKWAMISHA MAENDELEO.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdulla Juma Mabodi akikagua shamba la kuotesha miti mbali mbali ikiwemo ya Matunda huko Katika Kijiji cha Mungoni Wilaya ya Kusini Unguja.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdulla Juma Mabodi akiwa katika ziara ya katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja uliotekelezwa chini ya mpango wa ugatuzi.

Dk.Mabodi akizungumza na kuonyesha taarifa mbali mbali zinazofanyiwa uhakiki wa masuala mbali mbali ya utekelezaji wa ilani ya CCM.

 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdulla Juma Mabodi akikagua mradi wa utengenezaji wa Sabuni kwa kutumia mwani unaotekelezwa na Kikundi cha Wanawake cha ujasiriamali cha furahia kilichopo katika Kiji cha Paje.
 
 NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdulla Juma Mabodi akizungumza na Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa Kusini Unguja Mzee Haji Ussi Gavu mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Halmashauri ya Kusini Unguja.  

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Dk. Abdulla Juma Mabodi na viongozi wa Halmashauri na CCM wakikagua boti Maalum ya kusombea mwani  huko Paje.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  Dk. Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amesema endapo Wabunge na Wawakilishi watashindwa kutumia fedha za maendeleo ya mfuko wa jimbo zinazoingizwa katika Halmashauri za Wilaya, CCM itachukua hatua ya kuidhinisha fedha hizo zitumike kutatua kero sugu zinawakabili wananchi.

Msimamo huo ameutoa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 katika Halmashauri ya Wilaya Kusini Unguja, amesema fedha za mfumo wa maendeleo ya Jimbo ni haki ya wananchi na sio fedha za viongozi wa jimbo.

Amesema viongozi hao  wanakabidhiwa fedha hizo kwa ajili ya kusimamia utaratibu wa matumizi yake na sio kuziacha katika akounti za benki bila kutumika hali inayosababisha kutokamilika kwa baadhi ya miradi ya wananchi.

Dk. Mabodi akikagua miundombinu ya vyoo katika skuli ya Sekondari na Msingi ya Kusini Makunduchi alikuta skuli hiyo ina changamoto ya upungufu wa vyoo huku wanafunzi na walimu wakitumia vyoo chakavu, na kuamua kutoa agizo kwa Halmashauri kuidhinisha kiasi cha shilingi milioni 10 kutoka fedha za maendeleo ya jimbo hilo zilizokaa muda mrefu bila ya kutumiwa.

Pia Naibu Katibu Mkuu kupitia Ofisi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein aliahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni tano kwa ajili ya matengenezo ya haraka ya miundombinu ya vyoo hivyo kuhu akisisitiza viongozi wa Chama na Serikali kuchukua hatua za makusudi kumaliza changamoto za aina hiyo katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba.

Akiwa katika skuli hiyo alitoa wito kwa viongozi wa Chama na Serikali kushuka kwa wananchi hasa wa vijijini kuangalia changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kwa mujibu wa maelekezo yaliyomo katika Ilani ya CCM.

Aidha Dk.Mabodi akiwa katika shamba la kuotesha miti mbali mbali ikiwemo ya Matunda huko katika Kijiji cha Mungoni, alishauri wananchi wanaofanya shughuli hizo kuhakikisha wanaotesha miti inayotoa matunda yenye soko  ikiwemo miti aina ya midimu.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi wakati akikagua ukarabati wa Kituo cha Afya Mungoni aliitaka Halmashauri kuharakisha ujenzi huo ili wananchi waendelee kupata huduma bora za Afya.

Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu aliipongeza Halmashauri ya Kusini Unguja kwa kutekeleza vizuri miradi ya ujenzi wa vyoo na madarasa ya kisasa katika Skuli za Mtende na Bwejuu yaliyotekelezwa kupitia mpango wa ugatuzi wa madaraka kupitia Serikali za Mitaa.

Dk.Mabodi alimeridhishwa na hatua ya ukarabati wa skuli ya maandalizi ya Kijigoni Makunduchi   iliyotengenezwa kupitia mpango wa Ugatuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kusini.

Akizungumza Dk. Mabodi katika Kituo cha Afya Michamvi, aliagiza Halmashauri hiyo kuongeza majengo katika kituo hicho ili kiweze kuwahudumia wananchi wengi sambamba na kufanyiwa matengenezo nyumba ya Daktari awe anaishi karibu na kituo.

Akihitimisha ziara hiyo Dk.Mabodi kwa kumtembelea Mwenyekiti Msitaafu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, Mzee Haji Ussi Gavu ambapo Mzee huyo amepongeza juhudi za CCM Zanzibar katika kusimamia vizuri utekelezaji wa ilani ya CCM wenye lengo la kumaliza matatizo ya wananchi.

Dk. Mabodi alisema lengo la ziara hiyo kuwa ni kukagua miradi inayotekelezwa na Halmashauri pia anafanya uhakiki wa matumizi ya fedha za mifuko ya maendeleo ya jimbo zinazoingizwa katika halmashauri sambamba na kuibua kero za wananchi ili zifanyiwe kazi kwa wakati mwafaka.

“ Nampongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kwa kasi yao ya utekelezaji wa Ilani na mimi nitaenda na kasi yao kuhakikisha wananchi wananufaika na mipango ya maendeleo ya Serikali kwa kukagua miradi yote iliyotekelezwa na mpango wa ugatuzi”,. Alisema Dk.Mabodi.

Mapema akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kusini Unguja mwaka 2015/2018, alisema Halmashauri ilipanga kukusanya shilingi milioni 669,474,560 na imefanikiwa kukusanya mapato ya shilingi milioni 731,650,667 kipindi cha mwaka 2016/2018 sawa na asilimia 100.3.

Mkurugenzi huyo alieleza kwamba amesema wamewapatia mafunzo wakulima 92 ya utengenezaji wa dawa za asili za kuulia wadudu waharibifu wa mazao.

Sambamba na hayo wameongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani 177 mwaka 2016/2017 hadi tani 123 za mpunga kwa mwaka 2017/2018.

Pamoja na hayo Halmashauri imefanikiwa kuongeza uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi kutoka 967 mwaka 2014 kufikia 1,493 mwaka 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 54.3 .

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni