NA IS-HAKA OMAR,
ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’
amewatahadharisha wanachama wa chama hicho, kuwa makini kwa kuepuka propaganda
na njama chafu zinazofanywa na viongozi wakuu wa CUF waliotengeneza migogoro
bandia ili waweze kupata huruma ya wananchi kuingia madarakani.
Tahadhari hiyo
aliitoa wakati akimnadi mgombea wa nafasi ya Uwakilishi kwa tiketi ya CCM
Ramadhan Hamza Chande katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang’ombe huko katika
Uwanja wa Kwaalinatu.
Amesema CUF wametengeneza
mgogoro bandia wenye lengo la kuiyumbisha CCM mwaka 2020 mbinu dhaifu ambazo
hazitoweza kufanikiwa mbele ya CCM ya sasa iliyokuwa imara na inayokwenda
sambamba na ulimwengu wa siasa za Kisayansi.
Dk. Mabodi
amesema ushahidi pekee wa kuonyesha kuwa viongozi wa CUF hawana uadui kwa
upande wa Zanzibar na Tanzania bara ni pale waliposhirikiana kumnadi mgombea wa Chama hicho katika kampeni
za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Liwale ambao mgombea wa CCM ameibuka mshindi.
Akimnadi na
kumuombea kura Mgombea wa CCM katika Uchaguzi wa mdogo wa Jimbo la Jang’ombe
Ramadhan Hamza Chande, Dk. Mabodi amewasihi Wana-CCM na wananchi wa Jimbo hilo
kumchagua mgombe huyo ili aendeleze mambo mema yaliyoasisiwa na viongozi wa
waliopita wa nafasi hiyo.
Amesema CCM
imempitisha Ramadhan ikiamini kuwa ana uwezo na anafaa kutekeleza Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kasi kubwa.
Akieleza namna
Chama kilivyojipanga kuwaletea maendeleo Wananchi, Dk.Mabodi alisema CCM inafanya
siasa za kuimarisha maendeleo katika sekta zote Mijini na Vijijini ili kumaliza
ahadi zote zilizotolewa katika Uchaguzi mkuu uliopita kabla ya mwaka 2020.
Dk.Mabodi
ameongeza kuwa Chama kimekuwa kikishuka kwa wananchi wa makundi yote kwa lengo
la kuratibu changamoto na kuzitatua kwa wakati.
Naye Mgombea wa
tiketi ya CCM katika Uchaguzi mdogo wa Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande,
amewaomba wananchi na wanachama wa CCM wa jimbo hilo kukichagua Chama Cha
Mapinduzi kupitia mgombe huyo aweze kuwatumikia na kuharakisha maendeleo ya Jang’ombe.
Katika maelezo
yake Ramadhan amesema atakapopewa rdhaa na wananchi hao ya kuwa kiongozi
atashirikiana nao kupanga mikakati ya kupanga mikakati yenye tija ndani ya
Jimbo hilo.
Awali Mke wa Rais
mstaafu wa awamu ya nne ya Jamhuri ya Tanzania Mama Salma Kikwete, amesema matunda
yanayotokana na sera na mipango endelevu ya CCM yanaonekana wazi wazi kwani
Zanzibar na Tanzania bara zote zinang’ara kwa miundombinu ya kisasa ya barabara
na kuimarika kwa Sekta za Elimu, Afya pamoja na Maji safi na Salama.
Amesema CCM
imekuwa ikiendeleza misingi ya maendeleo iliyoasisiwa na Vyama vya ukombozi vya
ASP na TANU vilivyoungana na kuunda taasisi hiyo kwa nia ya kuongeza nguvu za
kusimamia ufanisi sera na mipango ya maendeleo kwa wananchi wote.
Akizungumza
katika Mkutano huo wa kampeni aliyekuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CUF Julius
Mtatiro aliyejiunga na CCM, amewaomba wananchi wa Jang’ombe kumchagua mgombea
wa CCM kwani vyama vya upinzani hasa CUF vina matatizo na migogoro isiyoweza
kutatulika kutokana na ubinafsi na sera za ubaguzi za viongozi wa vyama hivyo.
Mtatiro ametumia mkutano huo kuwaomba radhi Watanzania hasa Vijana wa CCM kuwa kipindi yupo
upinzani alitumiwa vibaya na CUF kukwamisha mipango ya maendeleo iliyokuwa
ikitekelezwa na Serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi.
Amesema kwa
kipindi cha zaidi ya miaka 10 aliyohudumu katika CUF, hakuna hata siku moja
Chama cha CUF ama UKAWA waliyoweza kushauri ama kupongeza mambo mema
yanayofanywa na CCM badala yake waliponda na kupotosha umma kwa makusudi.
Akizungumza Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Abdallah Hasnuu Makame, akimuombea kura mgombea wa CCM katika mkutano huo wa kampeni amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana yametokana uwepo wa tunu za Taifa ambazo ni Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Serikali mbili.
Amesema wananchi
wa Jimbo la Jang’ombe hawatojutia maamuzi yao endapo watamchagua mgombea wa CCM
aweze kuwaongoza kwa kipindi cha miaka miwili kufika 2020, kwani historia ya
siasa za Tanzania toka mwaka 1992 ulipoasisiwa mfumo wa vyama vingi CCM ndio
Chama pekee kilichoweza kutimiza kwa vitendo matakwa ya wananchi katika mfumo
wa vyama vingi.
Akizungumza
Mwakilishi wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Faida Mohamed Bakari,
amewaomba wanawake na vijana wa Jang’ombe kumchagua Ramadhan awe mwakilishi
kwani ana uwezo mkubwa wa kusimamia maslahi ya makundi hayo sambamba na
kuanzisha miradi mbali mbali itakayoweza kuwanufaisha wananchi.
Uchaguzi mdogo wa
Jimbo la Jang’ombe unatarajiwa kufanyika Octoba 27, mwaka 2018, kufuatia
aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Abdallah Diwani kuvuliwa uanachama kwa
makosa ya ukiukaji wa maadili ya Chama Cha Mapinduzi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni