Alhamisi, 8 Juni 2017

DR.MABODI NA BALOZI SEIF ALI IDD WASHIRIKI MAZISHI YA KADA MKONGWE WA CCM PEMBA.











Mwanasiasa Mkongwe wa Zanzibar Mzee Khamis Mkadara  aliyefariki Dunia mapemba jana asubuhi amezikwa Kijijini kwake Wawi Mkoa wa Kusini Pemba maziko yaliyohudhuriwa na Mamia ya Waumini wa Dini ya Kiislamu, Wananchi  pamoja na Viongozi wa Kiserikali na Kisiasa.   

Mzee Khamis Mkadara alikuwa akisumbuliwa na Maradhi ya kawaida pamoja na uzee alifariki nyumbani kwake Mtaa wa  Wawi Wilaya ya Chake chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika mazishi hayo aliiwakilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Chama cha Mapinduzi akijumuika  na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dr. Juma Abdulla Mabodi na baadhi ya watendaji wa Serikali.

Marehemu Mzee Khamis Juma Mkadara alizaliwa Mwaka 1927 na kuanza elimu ya Quran katika Madrasa mbali mbali za Wilaya ya Chake chake ambapo baadaye katika ujana wake akajishughulisha na masuala ya Kisiasa katika dhana nzima ya kudai Uhuru wa Visiwa vya Zanzibar.

Katika kipindi hicho ya kutaka kujikomboa Mzee Mkadara alikuwa muanzilishi wa Chama cha Shirazy Association na baadaye kukiunganisha na chama cha African Association na Kuzaliwa kwa Chama cha Afro Shirazy Party.

Katika utumishi wa Chama Mzee Khamis Juma Mkadara aliwahi kuwa Mwenyekiti wa ASP wa Wilaya ya Chake chake mwaka 1973 na baada  ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi mwaka 1977 aliendelea na wadhifa huo hadi mwaka 1997.

Mbali ya wadhifa huo wa Kichama Mzee Mkadara pia aliwahi kuwa Diwani wa Wadi ya Wawi mwaka 1995.

Mwanasiasa huyo mkongwe Kisiwani Pemba alikuwa mstawi wa mbele katika utetezi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akiwa miongoni mwa Wazee waliotumikia kwa kiindi kirefu Taifa hili la Tanzania.

Utumishi huo uliweza kumpatia fifa na ushujaa uliopelekea kutunukiwa nishani na Rais Mstaafu wa Tanzania Awamu ya Nne Dr. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Sita Dr. Aman Abeid Karume.

Mzee Khamis Juma Mkadara  aliyefikisha umri wa Miaka 90 ameacha Kizuka Mmoja, Watoto Wanane na Wajukuu 33.

Mwenyezi Muungu ailaze roho ya Mwanasiasa huyo Mkongwe Mzee Khamis Juma  Mkadara mahali pema peponi-Amin.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni