Mkufunzi wa Mafunzo hayo Bi.
Emiley Nelson Fwambo akizungumza na washiriki wa mafunzo ya
Wanawake na Uongozi katika siasa.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Abdulla Juma
Saadalla “ Mabodi” amesema CCM
itaendelea kufanya ushindani wa sera za maendeleo kisiasa zitakazowanufaisha wananchi
wa makundi yote mijini na vijijini.
Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mafunzo ya
Wanawake na Uongozi kwa wanachama na viongozi wa UWT Mkoa wa Mjini huko Amani
Zanzibar, Dkt. Mabodi amesema wananchi
wa visiwa vya Zanzibar kwa sasa wanachohitaji ni siasa za ushindani wa Sera za maendeleo na sio sera za vurugu na migogoro.
Dkt. Mabodi ameeleza kuwa taifa lolote linalotamani
kuendelea kiuchumi ni lazima wananchi wake wakubali kwa vitendo dhana ya siasa
za ustaarabu katika kudumisha amani na utulivu wa nchi ili kufanya kazi za
kujiongezea kipato katika hali ya Amani na utulivu.
Aidha Naibu
Katibu Mkuu huyo amesema ushindi wa CCM katika chaguzi mbali mbali za dola unatokana
na nguvu za Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi katika
kuunga mkono harakati mbali mbali za kisiasa hadi kuhakikisha chama kinaingia
madarakani.
“ kila mtu ndani ya Chama Chetu anajua na kutambua
mchango wa Wanawake katika medali za kisiasa, wao ndio wamekuwa mstari wa mbele
kwa kila kitu ikiwemo kujitokeza kwa wingi kupiga kura halali za kuiletea
ushindi CCM.
Pia naahidi kuwa nitakuwa nanyi bega kwa
bega kwa lengo la kuimarisha chama na jumuiza zake sambamba na kusimamia vyema serikali itekeleze Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili wananchi mpate maendeleo ya kudumu.”, amesema Dkt. Mabodi.
Kupitia
Mkutano huo Dkt. Mabodi amewasihi viongozi na
watendaji wa Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) kushuka ngazi za chini kiutendaji hasa matawi na mashina kwa lengo la kuratibu changamoto
zinazowakabili wananchi ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu na serikali.
Amewapongeza viongozi wa UWT waliojitolea kuanzisha mafunzo ya uongozi kwa wanawake wenzao
ili wapate ujuzi wa kufanya siasa za maendeleo zitakazowajengea ujasiri wa
kujenga hoja imara zinazokubalika katika ulimwengu wa siasa za ushindani.
Sambamba na hayo aliwapongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa
Zanzibar Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi kwa kutekeleza ipasavyo ilani ya Chama hicho hasa katika juhudi za kulinda rasilimali za nchi zisihujumiwe na baadhi ya watu wanaotanguliza mbele maslahi binafsi.
Akizungumzia Uchaguzi wa ngazi ya Wadi unaoendelea hivi
sasa katika Chama na Jumuiya Ameziagiza kamati zinazosimamia zoezi hilo
zifanye kazi ya ziada ya kuhakikisha wanapatikana viongozi safi wasiokuwa na
sifa za usaliti.
Mapema akizungumza katika Mkutano huo Mwenyekiti wa
UWT Mkoa wa Mjini, Bi. Waridi Juma
Othman aliahidi kuwa wanawake hao watatumia vizuri mafunzo ya uongozi katika
siasa kama muongozo wa kufanya kazi za kisiasa kwa ufanisi mkubwa.
Akitoa neno la shukrani Mbunge wa Viti Maalum wanawake( MNEC),
Khadija Hassan Aboud alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake
wa CCM ili waweze kuzitumika vizuri fursa za uongozi zinazopatikana ndani ya
chama na serikali kwa ujumla.
Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Mbunge wa Viti Maalum
wanawake( MNEC), Khadija Hassan Aboud kwa kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalum
Mkoa wa Mjini, Faharia Shomari Shomari Khamis kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake wa UWT ili wapate ukomavu wa kisiasa utakaosaidia CCM kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2020.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni