JUMUIYA ya Wazazi ya CCM Zanzibar imewataka watendaji wake wa ngazi mbali mbali za jumuiya hiyo kuwa waadilifu wakati wa kuchuja majina ya wagombea wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi kupitia uchaguzi unaoendelea ndani ya chama na jumuiya zake.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Bi.Nagma Giga wakati akikabidhi vitendea kazi ambavyo ni komputa na priter kwa Mikoa na Wilaya nane za jumuiya hiyo huko katika Afisi Kuu ya Wazazi Mpirani Kikwajuni Unguja.
Alisema watendaji wa ngazi za mikoa na wilaya za jumuiya hiyo ndio wasimamizi wakuu wa uchaguzi huo kwa ngazi mbali mbali za jumuiya hivyo wakati wa kuchuja wagombea ni lazima waweke kando urafiki na undugu na wawapitishe viongozi wenye sifa na uzalendo wa kukisaidia chama kushinda katika uchaguzi mkuu ujao.
“mafanikio tuliyonayo ndani ya jumuiya yrtu yanatokana na juhudi zenu za kiutendaji hivyo nakupongezeni sana na muendelee na kasi hiyo hiyo hadi tupate viongozi imara watakaotetea maslahi ya CCM mwaka 2020”,.alisema Giga.
Aidha aliwasisitiza viongozi hao kuhakikisha wanatunza vizuri vifaa walivyopewa na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kurahisisha shughuli za kiutendaji za jumuiya.
Akitoa neno la shukrani Katibu wa Wazazi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bi.Zaituni Bushiri Ussi aliahidi kuwa vifaa hivyo vitakuwa ni chachu ya kuharakisha maendeleo ya taasisi katika harakati za kiutendaji.
Vifaa hivyo ambavyo ni komputa nane zimekamilisha idadi ya komputa 19 ambazo Naibu Katibu Mkuu huyo aliahidi kutoa kwa Wilaya na Mikoa yote ya Jumuiya hiyo Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni