Jumatano, 7 Juni 2017

SALAMU ZA RAMBI RAMBI ZA CCM KUHUSIANA NA KIFO CHA MAREHEMU PROF. ISHAU ABDULLAH KHAMIS.


CHAMA Cha Mapinduzi kimepokea kwa mshituko, huzuni na masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha aliyewahi kuwa Mjumbe  wa Halmashauri Kuu na Afisa Mwandamizi (Mstaafu) wa Idara ya Organaizesheni CCM Zanzibar Marehemu Prof. Ishau Abdullah Khamis, kilichotokea tarehe 06 Juni, 2017, katika Hospitali ya Muhimbili, Mjini Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndg. Abdulla Juma Saadalla (Mabodi) kwa niaba ya Viongozi, Watumishi na Wanachama wote wa CCM, ametuma salamu za rambirambi kwa wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Mzee Ishau na kuwaomba kuwa na moyo wa subra katika wakati huu mgumu wa maombolezi yampendwa wetu huyo. Bila ya shaka kifo cha marehemu kimeacha pengo kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi na Taifa letu kwa ujumla.

Naibu Katibu huyo wa CCM Zanzibar amesema, Chama Cha Mapinduzi kimempoteza mwanachama mahiri, mchapakazi hodari, mpenda watu wa rika na jinsia zote na kwamba kifo chake kimekuja wakati Chama bado kinamhitaji kutokana na utumishi wake uliotukuka.

Katika uhai wake, na katika nyakati tofauti, marehemu Prof. Ishau Abdullah Khamis, aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Mkuu wa Mkoa, Mwalimu katika Chuo cha Uchumi (Dar), Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi na  Waziri wa Utalii na Misitu.

Kwa upande wa Chama marehemu aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Katibu wa Fedha, uendeshaji na Miradi ya Chama, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika Idara ya Organaizesheni - Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, cheo alichoshikilia hadi mwaka 2014, alipostaafu Utumishi wa Chama.


Kama hiyo haitoshi na kwa kutambua mchango wake mkubwa katika Utumishi wa Umma, mwaka 2016, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Takwimu ya Zanzibar, cheo ambacho alikuwa nacho hadi umauti ulipomfika.

Chama Cha Mapinduzi kinaungana na wanafamilia, ndugu na marafiki wa marehemu Tunamuomba Mwenyezi Mungu muumba Mbingu na Ardhi na Vyote viliomo ndani aiweke roho ya marehemu mahali pema Peponi. AMIN.


(Waride Bakari Jabu),
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
07/06/2017

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni