Chama cha Mapinduzi
(CCM) Zanzibar kimewataka Wabunge na Wawakilishi kisiwani Pemba kuwekeza katika
sekta ya elimu ili kuwasaidia vijana wanaosoma kwenye shule na vyuo vya elimu
ya juu vilivyopo katika kisiwa hicho.
Kauli hiyo imetolewa na
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi” katika
mwendelezo wa ziara yake Pemba wakati akikagua ujenzi wa shule ya Msingi na
Sekondari ya Kwale Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema viongozi hao wanatakiwa
kubuni miradi itakayosaidia kuinua viwango vya elimu kwa vijana mbali mbali
waliopo katika majimbo hayo ili waweze kupata taaluma zinakazowasaidia
kujiajiri wenyewe.
Ameeleza kuwa endapo kila jimbo litakuwa na wataalamu mbali
mbali waliosomeshwa na viongozi wa majimbo hatua hiyo itaongeza kasi ya
maendeleo kwa kupata wataalamu wa fani mbali mbali watakaohudumu kwenye sekta
za umma na binafsi katika majimbo hayo.
Sambamba na hayo aliwaagiza
Wabunge na wawakilishi hao kuongeza kasi katika kutatua kero zinazowakabili
wananchi ili kwenda sambamba na matakwa
ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Dkt.Mabodi alisema
viongozi hao wanatakiwa kuwa wa kwanza kuratibu changamoto zinazowakabili
wananchi kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kama walivyowaahidi wananchi
hao katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Pamoja na hayo amewapongeza
wananchi wa shehia ya Kwale Kisiwani Pemba kwa uzalendo wao wa kushiriki katika
shughuli za kijamii zikiwemo ujenzi wa Skuli ya Kwale ambayo kwa sasa wanasoma
watoto wa shehia hiyo na vitongoji vyake.
Kupitia ziara hiyo Dkt.
Mabodi amechangia shilingi milioni tatu kwa lengo la kusaidia ujenzi wa
madarasa ya shule ya Kwale.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni