Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Abdulla Juma Saadalla” Mabodi” akishiriki katika mazishi ya Marehemu Prof.
Ishau kwa kuweka udongo katika kaburi huko Wilaya ya Kaskazini "B" Donge.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein leo ameungana na mamia ya wananchi katika mazishi ya aliyewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu na Afisa Mwandamizi (Mstaafu) wa Idara ya Organaizesheni CCM Zanzibar , Prof. Ishau Abdullah Khamis huko kijijini kwao Donge Wilaya ya Kaskazini "B" Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Marehemu Prof. Ishau amefariki jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuuguwa kwa muda mrefu maradhi ya figo.
Katika mazishi hayo Dkt. Shein ameambatana na viongozi mbali mbali wa chama na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakiwemo Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Abdulla Juma Saadalla “Mabodi”
,Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi Mohamed, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, Katibu wa Mufti Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.
Prof.Ishau amepata elimu yake ya msingi katika Shule ya msingi Donge na kusoma elimu ya Chuo Kikuu Makerere Uganda na baadae kwenda nchini Hungry alikopata kiwango cha elimu ya Uprofesa na kurudi nchini kwa ajili ya kufanya kazi za umma.
Aidha Marehemu Prof. Ishau enzi za uhai wake aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo Mkuu wa Wilaya, Mkuu wa Mkoa, Ubunge, Mwalimu katika Chuo cha Uchumi (Dar), Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi na Waziri wa Utalii na Misitu.
Pia Prof.Ishau hadi kufariki kwake alikuwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ofisi ya Takwimu Zanzibar nafasi ambayo ameteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Kwa upande wa Chama marehemu aliwahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu, Katibu wa Fedha, uendeshaji na Miradi ya Chama, Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika Idara ya Organaizesheni - Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, cheo alichoshikilia hadi mwaka 2014, alipostaafu Utumishi wa Chama.
Chama Cha Mapinduzi kinaungana na wanafamilia, ndugu na marafiki wa marehemu Tunamuomba Mwenyezi Mungu muumba Mbingu na Ardhi na Vyote viliomo ndani aiweke roho ya marehemu mahali pema Peponi amin.
Marehemu amefariki akiwa na umri wa miaka 75 na ameacha watoto Sita.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni