UNAPOZUNGUMZIA dhana ya maendeleo endelevu katika Ulimwengu wa sasa wa karne ya 21 iliyotawala Sayansi na Teknolojia, huwezi kukosa kuitaja miundombinu ya usafiri na usafirishaji hasa babaraba za kisasa zilizojengwa kwa kiwango cha lami.
Sekta hiyo imekuwa ni moja ya kichocheo kikubwa cha shughuli za kiuchumi ambazo zinawezesha pia kuongeza ajira nchini.
Pia urahisisha shughuli za usafirishaji wa mazao na bidhaa mbali mbali za kibiashara kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa haraka zaidi na bila kutokea madhara yoyote kwa bidhaa zinazosafirishwa.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Mohamed Shein imeendelea kuwekeza kwa kiasi kukubwa katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kisasa ya barabara Unguja na Pemba, ambazo zimekuwa msingi mkubwa wa kukua kwa uchumi na shughuli nyingene za kijamii.
Zanzibar imepiga hatua kubwa katika sekta hii na kuifanya kuwa moja kati ya nchi chache katika Barani Afrika zenye mitando bora na imara ya miundombinu ya usafiri hasa barabara.
Kupitia kampeni za Uchaguzi mkuu uliopita Chama cha Mapinduzi(CCM) ilinadi Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote na kuahidi kutengeneza barabara za kisasa mijini na vijijini ili kupunguza ukali wa maisha ya wananchi.
Dk. Shein sio tu kwamba amefanya mapinduzi makubwa ya kuimarisha sekta ya barabara pekee bali yapo mengi aliyoyatekeleza kwa kipindi kifupi cha utawala wake katika mitando mbali mbali ya miundombinu ikiwemo Viwanja vya ndege, usafiri wa baharini na zingine nyingi.
Licha ya juhudi hizo bado baadhi ya watu wanaolazimisha ‘upofu wa macho’ na kuondokewa na dhana ya utu na uzalendo katika mioyo yao kwa kujifanya hawaoni wala kutambua Sera za kimaendeleo zinazotekelezwa na Serikali sikivu ya CCM.
Tunajua binadamu wote hatupo sawa kifikra na kivitendo licha ya hapa kwetu kuwepo baadhi ya vyama vya kisiasa wamejivisha joho la kupakazia ubaya wa kila jambo linalotekelezwa na upande wasiouamini wao. Siasa hizo hakika zimepitwa na wakati katika zama hizi za ‘Kidigital’.
Hata kama yanayofanyika kwao wao ni sawa na mwiba kuwachoma lakini sharti ni lazima wayathamini na kuyakubali japo kwa kimya kimya kwani yanatekelezwa kwa maslahi ya umma na sio kwa matakwa ya mtu binafsi wala chama fulani.
Nakumbuka kichwa cha habari kutoka katika moja ya Gazeti linalopendwa hapa nchini kiliwahi kusema kuwa ‘Kasi ya Dk.Shein katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ni mwiba kwa wapinzani’, hakika maudhui ya habari hiyo yalijieleza kwa upana kwa kuonyesha uhodari wa Rais huyo ambaye ni mungwana anayeahidi na akatenda kwa vitendo.
Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kwa kushirikiana na watendaji na viongozi wa Chama na serikali Zanzibar wamekuwa wakikesha wanawaza na kubuni mikakati mbali mbali ya kuwaletea maendeleo wananchi zikiwemo kutafuta wahisani wa kimaendeleo kutoka taasisi za kimataifa ili wasaidie kutoa msaada wa kutekeleza baadhi ya miradi.
Siku mbili zilizopita Serikali imetiliana saini Mkataba wa Ujenzi wa Bara Nne za Bububu- Mahonda- Mkokotoni, Pale Kiongele, Matemwe – Muyuni na Fujoni – Kombeni zinazotarajiwa kuwa na urefu wa Kilomita 52.
Mkataba huo uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “A” uliopo Mkokotoni ulishuhudiwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Kisiasa wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Saini ilitiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Nd. Mustafa Aboud Jumbe wakati ule wa Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China (CCECC) inayojenga Bara bara hizo ulitiwa na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Nchini Tanzania Bw. Jiang Yi Giao.
Ujenzi wa Mradi huo wa Bara bara ambao ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015 -2020 unagharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mkopo nafuu wa fedha wa Shilingi Bilioni 58 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).
Akizungumza mara baada ya utiaji saini Mkataba huo wa Ujenzi wa Bara bara Nne za Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar isingependa kuona inaingia katika migogoro na Wajenzi wa Miradi tofauti.
Balozi Seif alisema zipo Kampuni zilizowahi kutiliana saini Mikataba ya Ujenzi wa Miundombinu ya Bara bara na hatimae Kampuni hizo zikaingia mitini na kushindwa kukamilisha Mikataba ya Miradi waliyoikubali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi watakaohusika na maeneo yatakayopita Miradi hiyo ya Bara bara wasaidie kuharakisha Miradi hiyo ili imalizike kwa wakati uliopangwa.
Alisema changamoto za ulipaji wa fidia za Majengo pamoja na vipando vya Wananchi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi huo isiwe vikwazo vya kuviza mpango wa Maendeleo uliokusudiwa kufanywa na Taifa.
Mapema Kaimu Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Mradi huo wa Bara bara utahudumia watu wote bila ya ubaguzi au itikadi za Kisiasa.
Hivyo Mh. Ayoub alionya kwamba Mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuzuia kuendelea kwa miradi hiyo Serikali haitosita kumchukuliua hatua zinazofaa za kinidhamu.
Alisema ni vyema kwa Wananchi wawe tayari kuipokea miradi hiyo sambamba na kushirikiana na Serikali pamoja na Wajenzi wa Mradi huo ili kuhakikisha inafanikiwa na kuleta tija kwa Jamii yote Nchini.
Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Balozi Ali Karume alisema kuimarika kwa Miundombinu ya Bara bara Nchini ni chachu ya Maendeleo kwa Taifa.
Balozi Karume alisema usumbufu wa usafiri kwa Wananchi wanaoishi katika maeneo utakayopita Mradi huo unatarajiwa kuwa Historia baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Bara bara hizo.
Waziri wa Ujenzi, Miundombinu na Usafirishaji aliwaomba Wajenzi wa Mradi huo kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China (CCECC) kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa wakati uliomo kwenye Mkataba wa Ujenzi.
Akitoa salamu za Kampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi ya China (CCECC) Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Tawi la Tanzania Bwana Jiang Yi Giao aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Utaalamu na uzoefu iliyonayo Kampuni hiyo ndio shahada inayothibitsha wazi kwamba kazi za Taasisi hiyo zinafanywa kwa sheria na Taratibu zilizopo.
Jiang alisema Kampuni ya CCECC iliyoasisiwa mnamo mwaka 1979 tayari ina uzoefu mkubwa uliopelekea kuwa miongoni mwa Makampuni ya Kimataifa ya Uhandisi wa Ujenzi 100 yaliyopo Duniani.
Alisema Kapuni hiyo ya ujenzi imeshakuwa maarufu Duniani likiwemo Bara la Afrika ambapo Miradi mbali mbali imeshajenga ikiwemo Reli ya Tanzania na Zambia, Bara bara na Madaraja ya kisasa katika Miji mingi Barani Afrika yakiwemo Majengo makubwa ya huduma za Jamii pamoja na Kijiji cha Kisasa Nchini Rwanda.
Aidha Jiang alifafanua kwamba (CCECC) pia imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi ya Kijamii kwa Wananchi wa Mataifa yanayofunga Mikataba ya Ujenzi wa Miradi tofauti ya Maendeleo na Kampuni hiyo.
Bara bara ya Bububu –Mahonda – Mkokotoni itajengwa na kupanuliwa upana wa Mita 8 wakati nyengine Tatu zilizobakia zitajengwa kwa upana wa Mita 6 chini ya usimamizi wa Taasisi ya Gauff kutoka Nchini Ujerumani.
Wakizungumza kwa wakati tofauti baadi ya wananchi wa maeneo yanayojengwa barabara hizo waliipongeza serikali kwa juhudi zake za kuwajali wananchi kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za kijamii.
Akizungumza mkaazi wa kijiji cha Matemwe Mariam Foum Mansour, alisema ujenzi wa barabara hizo ni miongoni mwa fursa za kimaendeleo zitakazowasaidia wananchi wa kijiji hicho kupata urahisi zaidi wa kutekeleza shughuli za kimaendeleo na kiuchumi.
Salum Khamis Ameir ambaye ni mkaazi wa Bububu alipongeza hatua zilizofikiwa na SMZ kwa kuonyesha nia ya kuanza ujenzi wa barabara hizo na aliongeza kuwa ni wakati mwafaka wa kuboresha miundominu hiyo kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya babaraba hiyo.
“ Mimi ni mfuasi wa Chama kimoja cha upinzani hapa Zanzibar ambaye wakati serikali inatekeleza miradi ya maendeleo kwa jamii ushabiki wangu naweka pembeni , lakini lazima niwe muwazi kwa kasi hii ya Dk.Shein na Dk.Magufuli yawezekana wapinzani wengi kabla ya 2020 tukajiunga na CCM.”, alisema Salum.
Utekelezaji mzuri wa Sera za maendeleo za CCM ndio kipimo sahihi cha Chama makini chenye dhamira ya kweli ya kutatua kwa haraka kero na changamoto zinazowakabili wananchi wote.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni