Jumanne, 7 Novemba 2017

CCM Z'BAR YASEMA MIAKA MIWILI YA DK.MAGUFULI MADARAKANI UCHUCHUMI UMEIMARIKA.


 KATIBU WA KAMATI MAALUM YA NEC, IDARA YA ITIKADI NA UENEZI CCM Z'BAR BI.WARIDE BAKARI JABU.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka viongozi na watendaji wa Chama na Serikali kufuata nyayo za kiutenda za Rais Dk John Pombe Magufuli katika kupigania maslahi ya wananchi hasa wa kipato cha chini.

Rai hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,  Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar , Waride Bakari Jabu wakati akizungumzia miaka miwili ya Utawala Dk. Maguful huko Afisini kwake Kisiwandui Unguja,  amesema  Rais huyo ametekeleza mambo mengi ya kimaendeleo yanayotakiwa kuigwa na kuenziwa na viongozi wengine nchini.

Alieleza kuwa juhudi zinazofanywa na Dk.Magufuli katika kusimamia vizuri matumizi ya rasilimali za nchi ni miongoni mwa sera za Chama cha Mapinduzi katika kusimamia haki, usawa na mali ili ziwanufaishe wananchi wote.

Waride alisema CCM Zanzibar inapongeza hatua  za kimaendeleo zilizofikiwa nchini kutokana na juhudi za Rais huyo katika kusimamia vizuri rasilimali za nchi hatua inayochangia kuwepo  kwa uwiano wa  ukuaji wa uchumi baina ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alieleza kuwa utendaji huo wa serikali toka imeingia madarakani umekuwa ni miongoni mwa ajenda za kitaifa na kimataifa inayoiletea sifa nyingi CCM ambayo ndio inayosimamia utekelezaji wa Ilani yake kwa ufanisi mkubwa kwa wananchi wote bila ya ubaguzi.

Katibu huyo  alisema ujasiri na uthubutu aliouonyesha Rais wa kuwashughulikia wafanyakazi hewa, watumishi wenye vyeti bandia, kuwatumbua watendaji wazembe na wengine kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ubadhirifu na uhujumu uchumi , umefungua ukurasa mpya wa ajabu .

“ CCM Zanzibar tunampongeza Dk.Magufuli na wasaidizi wake kwa kutimiza miaka miwili yenye mafanikio madarakani ambapo tunamuahidi kuwa tutamuunga mkono na kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa maagizo yake kwa upande wa Chama na Serikali kwa ujumla.

Pia utendaji wake uliotukuka ni miongoni mwa mambo yanayoleta faraja na hamasa kubwa kwa wananchi kuendelea kuamini na kuiunga mkono CCM ambacho ndio chama anachotekeleza sera zake”, alieleza Katibu huyo Bi.Waride na kuwasihi wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa kumuunga mkono Rais huyo.

Akizungumzia baadhi  ya mambo ya  kihistoria yaliyotekelezwa  na Dk. Magufuli katika utawala wake kuwa ni pamoja na kufufua shirika la ndege, kununua ndege mpya, kuanzisha ujenzi wa reli ya kutumia umeme, kuongeza mapato ya kodi, miradi ya gesi na umeme kama ule wa steagles Garge huko Rufiji  na kushughulilikia mikataba mibovu ya madini.

Bi. Walide alimtaja Dk.Magufuli kuwa ni kiongozi shujaa aliyepambana na vinara wa ufisadi waliokuwa wakihujumu maendeleo ya nchi na kujilimbikizia mali huku wananchi wakiteseka kwa kukosa hata huduma za msingi katika sekta za elimu, afya na miundombinu.

Hata hivyo Katibu huyo alisema ndani ya kipindi cha miaka miwili iliopita serikali imedumisha mahusiano mema na nchi jirani, nchi wahisani na washirika wa maendeleo pia kushughulikia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu .

Kwa upande wa kisiasa alisema Rais  Dk. Magufuli  ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa mara baada ya kukabidhiwa dhamana hiyo alianza mikakati ya kuimarisha Chama kwa kufanya mabadiliko ndani ya Katiba ya CCM ili kwenda na wakati wa sasa kisiasa huku akisisitiza sera ya chama hicho kujitegemea kiuchumi kwa kuendeleza na kuanzisha miradi mipya itakayoleta manufaa kwa wanachama wote wa chama hicho.

Dk. Magufuli aliwasihi Rais Magufuli wananchi na viongozi wa kisiasa kuweka kando itikadi za vyama badala yake wajali uzalendo na maendeleo katika kubadili sura ya nchi toka kwenye wimbi la umasikini na kuwa taifa huru lililoendelea kiuchumi.

 Pamoja na hayo Bi.Waride, alisema juhudi za kiongozi huyo katika kukijenga Chama na Jumuiya zimeanza kuonekana katika Uchaguzi unaoendelea hivi sasa ndani ya taasisi hiyo  kwa kuthibiti wanachama wanaowania uongozi wenye sifa za rushwa, makundi na safu za kuhatarisha chama kuhakikisha hawapewi uongozi kwa lengo la kuwapata viongozi bora na waadilifu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni