Jumanne, 28 Novemba 2017

UWT NGAZI ZA MIKOA ZANZIBAR WAFANYA UCHAGUZI

Na Is-haka Omar , Zanzibar.

JUMUIYA ya Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) ngazi za Mikoa ya Zanzibar leo wamefanya uchaguzi wa kuwapata viongozi mbali mbali watakaoongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Akizungmza katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais Mama Asha Suleiman Idd,uliofanyika katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, amewataka wagombea ambao watashinda katika nafasi mbalimbali kuwa chachu ya kuendeleza Umoja na mshikamano ndani ya jumuiya hiyo.


Alisema uchaguzi huo ni muhimu kwa kila mwanachama wa  jumuiya hiyo kwani viongozi watakaochaguliwa ndio wenye dhamana ya kuunda jeshi la kisiasa litakalofanikisha ushindi wa CCM mwaka 2020.

Hata hivyo amewasihi wagombea watakaoshindwa katika uchaguzi huo wawe na subra na wasiinunie jumuiya wala kukisusia Chama kwani uongozi unatokana na majaliwa ya mwenyezi Mungu.

 Amesema uchaguzi si uhasama na kwamba baada ya mchakato huo kuisha kinachotakiwa ni kuendelea kushikamana kwa ajili ya ushindi wa mwaka 2020 wa CCM.
 Aliongeza kwa kufafanua kuwa haina maana wagombea hao kukinunia chama ama kususa kutokana na ushindani ulioko ndani ya jumuia.

Katika maelezo yake Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais, alisema kinachotakiwa katika uchaguzi huo ni kuwapata viongozi wapiganaji ambao watafanya kazi kwa pamoja ili kuleta mabadiliko makubwa katika jumuia hiyo.

“Maendeleo ndani ya UWT yataletwa na wanawake wa CCM na sio taasisi wala watu wengine, hivyo tuendelee kutumia nguvu na ushawishi tulionao kuhakikisha miaka mitano ijayo jumuiya inakuwa na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo.

 Wagombea hao wanapaswa kutambua kuwa lazima wakubaliane na matokeo ya uchaguzi ambao wajumbe watawachagua kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa chama. ” Alisema Mama Asha.

Aliwataka akina mama hao kuwashawishi idadi kubwa ya wanawake kuingia ndani ya CCM na kwamba wajiulize chama wamekifanyia nini jibu lake ni kukiongezea nguvu kubwa kwa kwavuta wanachama wapya kujiunga na Chama.

Mbali na nasaha hizo, alieleza kuwa matokeo ya ushindi wa uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata mbali mbali huko Tanzania Bara unatokana na sera ya Rais Dk.John Magufuli aliyoingianao hivyo ni vyema UWT mkoa huo ujitathmni na kuhakikisha wanafanya mikakati ya ushindi wa mwaka 2020.

“Tujifunze kuwa siasa zetu za huku na za Bara tofauti hivyo tujifunze kuwa watu wanataka maendeleo na si huku watu wanamtaka mtu ndio maana sasa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani umejionesha wazi hivyo sisi kazi yetu huku ni kuonesha na kuwashawishi wananchi waone maendeleo yanayofanywa na CCM ili iwei rahisi katika ushindi wa mwaka 2020,”alisema.

Kwa upande wake Mjumbe wa Baraza Kuu UWT, Panya Ali Abdalla, aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuhakikisha wanachagua viongozi madhubuti ambao watakisaidia chama katika kuleta mabadiliko ndani ya chama na jumuia hiyo.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Kaskazini, ambaye muda wake umekwisha, Miza Ali Kombo, alisema wajumbe ambao watapiga kura katika uchaguzi huo ni 129 na kwamba waliohudhuria ni 118 katika majimbo tisa ndani ya mkoa huo.

Mapema Akifungua Mkutano Mkuu wa UWT, Mkoa wa Mjini Unguja, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma aliwataka wajumbe wa mkutano huo kuwachagua viongozi bora wasiokuwa na makundi ya kuhatarisha uhai wa chama na jumuiya hiyo.

Aliwataka viongozi watakaoshinda katika uchaguzi huo wahakikishe wanakwenda sambamba na kasi ya utendaji wa CCM katika kusimamia vizuri utekelezaji wa sera zake kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu wa UWT Mkoa wa Kusini Unguja, Sitamili Omar  Dendego alisema uchaguzi umefanyika vizuri katika mkoa huo na wanatarajia kuwapata viongozi watakaolinda maslahi ya jumuiya na CCM kwa ujumla.

Uchaguzi huo uliofanyika katika Mikoa yote ya UWT Zanzibar na Tanzania kwa ujumla nafasi ambazo zinashindaniwa  ni Wenyeviti wa Mikoa, Wajumbe wa Baraza kuu Taifa nafasi nne,Wajumbe wa Baraza Kuu Mkoa nafasi 10, Mwakilishi wa Umoja wa Vijana(UVCCM) nafasi moja na Jumuia ya Wazazi nafasi moja.
Mke wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mama  Asha Suleiman Idd akifungua mkutano mkuu wa UWT Mkoa wa kaskazini Unguja.

 Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UWT Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 Baaadhi ya Wajumbe wa  Mkutano Mkuu wa  UWT Mkoa wa Mjini Unguja.
Baadhi ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu  wa UWT Mkoa wa Kusini Unguja wakifuatilia kwa umakini mchakato wa uchaguzi unaoendelea katika Mkoa  huo.

Mjumbe kutoka kundi la Vijana akiomba kura katika Mkutano Mkuu wa  UWT Mkoa  wa  Kusini Unguja.





    

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni