Ijumaa, 24 Novemba 2017

DR. MABODI ASISITIZA MABADILIKO YA KIUTENDAJI KWA WATUMISHI



Na Is-haka Omar, Zanzibar.
         

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimewataka watumishi wake kubuni mikakati   endelevu itakayoleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo ndani ya Chama katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.


Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar , Dk. Abdulla Juma Mabodi jana wakati akifunga mafunzo elekezi ya siku moja kwa watendaji wa Afisi Kuu CCM Zanzibar, yaliyofanyika Kisiwandui Unguja.

Alisema Watendaji ndio nyenzo muhimu ya kuleta maendeleo ndani na nje ya Chama hicho  ili kiendelee kuwa kinara wa Demokrasia iliyotukuka na Sera zenye manufaa kwa wananchi wote.

Dk. Mabodi alieleza kwamba dhamira ya mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watendaji hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“ Baada ya mafunzo haya natarajia kuona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika shughuli zenu za kila siku, kwani mmepewa ujuzi na maarifa mapya yatakayosaidia kuzikabi changamoto na kuzigeuza kuwa ni fursa za kuijenga CCM Mpya na Tanzania mpya’’. alisema Dk. Mabodi.

Naye  Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Organizesheni, Haji Mkema Haji aliwambia washiriki wa mafunzo hayo kuwa wanatakiwa kujituma na kufanya kazi kwa bidii ili watendaji na watumishi wa ngazi zingine za chama na jumuiya wajifunze kwao.

Akiwasilisha mada ya muundo wa CCM na namna unavyofanya kazi, Mkufunzi kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma, Filbert Mdaki Mampwepwe  alisema chama hicho ni zao la muungano wa vyama vya ukombozi vya ASP na TANU, hivyo ni wajibu wa kila mwanachama kulinda na kutetea urithi huo popote bila hofu.

Alieleza kwamba toka kuzaliwa kwa chama hicho 5 februari, 1977 kimepitia katika mabadiliko mbali mbali ya kisera na kimuundo yenye malengo ya kwenda sambamba na matakwa ya Katiba ya CCM na Kanuni zake.

“ Waanzilishi wa vyama hivi ambao ni marehemu Baba wa Taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Shekhe Abeid Amani Karume watakumbukwa daima kama mashujaa wa Taifa hii lenye historia ya pekee barani Afrika.”, alieleza Makeko.

Kwa upande wake Mkufunzi kutoka Makao Makuu ya CCM,  Ali  Juma Makoa akiwasilisha mada ya majukumu na kazi za Idara ya Uchumi na Fedha,  alifafanua kwamba dhamira ya Idara ni kuifanya CCM kuwa taasisi yenye nguvu kiuchumi, ikiwa na Mapato ya kutosha kugharamia shughuli zake zote ikiwemo chaguzi na kutoa maslahi mazuri kwa watendaji wake.

Aliongeza kuwa kila mwanachama bila kujali cheo wala nafasi aliyonayo ndani ya Chama anatakiwa kulinda na kuheshimu rasilimali mbali mbali za taasisi hiyo, zisihujumiwe na watu wachache badala yake zitumike kwa malahi ya wanachama wote.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliahidi kuyafanyia kazi kwa vitendo katika sehemu zao za kiutenda kwa lengo la kuimarisha uhai wa Chama.

Mafunzo hayo yaliyowashirikisha Watendaji wa Idara na vitengo vyote vya CCM Zanzibar, yalikuwa na mada nne zikiwemo Majukumu na Kazi za Idara ya Uchumi na Fedha, Muundo wa CCM na namna unavyofanya kazi, Majukumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi pamoja na Umuhimu wa kuzingatia maadili kwa Watumishi na Viongozi wa Chama.

Baadhi ya washiriki wa Mafunzo elekezi kwa Watumishi wa CCM Afisi  Kuu Zanzibar wakifuatilia kwa makini mafunzo hayo yaliyofanyika katika katika Ukumbi wa Ofisi hiyo Kisiwandui Unguja.











Hakuna maoni:

Chapisha Maoni