Mashine ya Kisima cha Maji safi na Salama katika Skuli ya Kitope iliyoharibika
hivi karibuni na kwa sasa inayofanyiwa matengenezo ili wananchi wa maeneo hayo
waweze kuendelea kupata huduma ya maji.
|
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi
akiangalia sehemu iliyoibiwa waya wa umeme katika Kituo namba 4 kisima
kilichopo eneo la Kiashange Wilaya ya Kaskazini “A”. (PICHA NA AFISI KUU ZANZIBAR).
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimekemea vitendo vya kuhujumu miundombinu ya maji safi
na salama vinavyofanywa na baadhi ya watu wenye nia ya kukwamisha juhudi za serikali
katika kuwapelekea wananchi huduma muhimu za kijamii.
Akizungumza Naibu Katibu Mkuu
wa Chama hicho Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi katika ziara Maalum ya kukagua
baadhi ya maeneo yaliyohujumiwa miundombinu hiyo katika Mkoa wa Kaskazini
Unguja huko katika shehia ya Mkwajuni katika Kisima namba 4 cha Kiashange Wilaya ya Kaskazini “A”.
Alisema Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar imekuwa ikitumia fedha nyingi za walipa kodi kuimarisha miundombinu
ya maji mijini na vijijini ili wananchi waondokana na kero ya ukosefu wa huduma
hiyo lakini kuna baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi wamekuwa wakiharibu miundombinu hiyo kwa makusudi.
Kisima hicho kilichoibiwa waya za umeme wa mashine inayosukuma maji hadi tangi kubwa la Kijiji cha Nungwi na maeneo jirani linalosambaza maji katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Kaskazini “A” hali inayosababisha usumbufu kwa baadhi ya wananchi wa maeneo hayo.
Kisima hicho kilichoibiwa waya za umeme wa mashine inayosukuma maji hadi tangi kubwa la Kijiji cha Nungwi na maeneo jirani linalosambaza maji katika maeneo mbali mbali ya Wilaya ya Kaskazini “A” hali inayosababisha usumbufu kwa baadhi ya wananchi wa maeneo hayo.
Dk.Mabodi alieleza kwamba maji yana mahitaji muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu hivyo
yanapokosekana ama kutopatikana kwa wakati yanasababisha usumbufu na madhara
makubwa hasa katika maeneo ya huduma za kijamii yakiwemo Nyumba za Ibada, Hospitalini, Shuleni na kwa wagonjwa wanaotibiwa wakiwa majumbani mwao.
Alisema vitendo vya kuziba mipira ya maji kwa kutumia zege,
kuiba mipira, mabomba, pumbu, mashine za kusambazia maji, waya za umeme, Transfoma pamoja
kufunga mifugo katika maeneo ya miundombinu ya maji ni vitendo hivyo ni miongoni mwa hujuma zisizokubalika kisheria na kijamii.
Naibu Katibu Mkuu huyo
alifafanua kuwa CCM miongoni mwa majukumu yake ni kuisimamia serikali itatue
kero za wananchi hivyo haitokuwa tayari kuona vinafanyika vitendo vya kuharibu
hali ya kisiasa na amani ya nchi kwa kuharibu kwa makusudi rasilimali za nchi katika
Mkoa huo.
Alitoa wito kwa wananchi wa maeneo
mbali mbali yenye miundombinu ya maji katika Mkoa huo kuhakikisha wanakuwa
walinzi wa rasilimali hizo na kutoa taarifa sahihi kwa Mamlaka ya Maji Zanzibar
(ZAWA) ili wawachukulie hatua za kisheria watu wanaijihusisha na hujuma hizo.
Ameagiza viongozi wa CCM wa ngazi za Wilaya na Mkoa
wa Kaskazini Unguja kukaa karibu na wananchi kuibua kero zao na kusimamia
utekelezaji wa ilani ya uchaguzi unaofanywa na serikali.
Pia amehimiza
serikali kukamilisha taratibu za upatikanaji wa huduma za maji kutoka
katika visima vilivyochimbwa na wadau wa maendeleo ili viwasaidie wananchi kupata huduma za maji kwa uhakika.
Pamoja na hayo Dk. Mabodi ameishauri serikali
kuanzisha mpango wa kutengeneza matangi makubwa ya maji katika shehia na zoni
mbali mbali nchini.
Hata hivyo amezitaka Kamati za maendeleo za shehia
zenye tatizo la maji huko Kitope kukaa
kimkakati na watendaji wa Wizara inayoshughulikia maji na nishati ya umeme
kuhakikisha umeme unapatikana muda wote katika miundombinu ya maji.
Naye Kaimu Afisa wa Maji wa Mkoa
huo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Dude
Juma Ame alishauri kuwekwa walinzi
katika maeneo mbali mbali yenye miundombinu ya maji katika Mkoa huo ili
kudhibiti hujuma hizo.
Mapema akizungumza Naibu Katibu
Mkuu huyo Dk. Mabodi katika Kisima cha
maji kilichopo maeneo ya Kitope Skuli ambacho hakitoi maji kutokana na kuharibika kwa kifaa ndani ya Pampu ya kisima
hicho aliwataka mafundi wa Mamlaka ya Maji
Zanzibar (ZAWA) kuharakisha matengenezo hayo ili wananchi wa maeneo hayo
waendelee kupata huduma za maji.
Kutokana na mahitaji ya huduma
ya maji safi na salama katika Hospitali ya Kitope, Dk. Mabodi
alisema CCM Zanzibar itachimba
kisima cha maji safi na salama ndani ya hospitali hiyo ili wapate huduma hiyo
kwa wakati mwafaka.
Akitoa ufafanuzi juu ya
matengenezo ya Pambu ya Kisima hicho Afisa wa Wilaya ya Kaskazini “B” Unguja, Amour
Mohamed Silima alisema kuwa vifaa vinavyohitajika tayari vimeshapatikana hivyo
kufikia kufikia mwezi Novemba 4,
mwaka huu watakuwa wamekamilisha na wananchi wanapata huduma ya maji.
Alifafanua kuwa changamoto
inayowakabili katika visima vya maji mbali mbali ndani ya Wilaya hiyo ni
kuharibika kwa mashine za maji kutokana na athari za umeme zinazosababishwa na
madhara ya Radi katika kipindi cha msimu wa Mvua za vuli zinazoendelea kunyesha
nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni