Jumapili, 12 Novemba 2017

UVCCM JIMBO LA MALINDI WAAGIZWA KUANZISHA MIRADI YA MAENDELEO


UONGOZI wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Jimbo la Malindi umeagizwa kukutana na Kamati ya Utekelezaji ya Jimbo hilo kubuni Miradi ya maendeleo itakayowanufaisha Vijana. 


Agizo hilo limetolewa  na Mwenyekiti wa UVCCM  Wilaya ya Mjini, Huzaima Mbarouk Tahir wakati akihimisha ziara yake kwa majimbo yote ya Wilaya hiyo yenye lengo la kuimarisha uhai wa Umoja huo.


Alifafanua kuwa Umoja huo unatakiwa kutumia Kikao cha   Kamati ya utekelezaji  kwa kushirikiana na viongozi akiwemo Mwakilishi kujadiliana na kuandaa miradi itakayosaidia kupunguza changamoto zinazowakabili vijana.  


Kwa upande wake Mwakilishi wa Jimbo hilo, Mohamed Ahmada Salum ambae pia ni Naibu waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Alieleza kuwa Ofisi yake imesaidia  gharama za masomo ya ujasiria mali na Ufundi kwa Vijana 71 jimboni humo.


Alisema hatua hiyo ni miongoni mwa Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM aliyotekeleza kwa kipindi cha mwaka 2016/2017.


“ Nimepanga mikakati mbali mbali ya kuwasaidia vijana hasa walioshindwa kuendelea na elimu ya juu kuhakikisha wanapata elimu ya Ufundi itakayowasaidia kujiajiri wenyewe”, alisema Mohamed. 


Aliwataka vijana kutumia fursa zilizopo ndani ya Jimbo  kwa kujiunga katika Vikundi rasmi ili iwe rahisi kuwatambua na kuwapatia mitaji ya kuanzisha ujasiria mali.


Ziara hiyo ya UVCCM ngazi ya Wilaya ilianza Rasmi  Novemba 4  mwaka huu katika Jimbo la Kikwajuni, Jang’ombe, kwahani na leo hii imefika tamati katika Jimbo la Malindi ambapo zaidi ya Vijana 28 wamekabidhiwa kadi za Umoja huo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni