Jumapili, 12 Novemba 2017

ABDULGHAFAR- AWAPIGA MSASA BARAZA KUU UVCCM WILAYA YA MFENESINI

 
KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Abdulghafar  Idrissa Juma amewataka viongozi wa Baraza kuu la UVCCM Wilaya ya Mfenesi kuwa sehemu muhimu ya kuwaunganisha vijana na sio kuwagawa katika makundi yatakayoweza kuleta migogoro ndani ya Umoja huo.

Rai hiyo ameitoa leo wakati akifungua Kikao cha kwanza cha Baraza hilo uliofanyika katika Ofisi za UVCCM Mfenesini zilizopo Bububu Unguja.

Alisema wajumbe wa Baraza hilo wanatakiwa kuwa mstari wa mbele kushughulikia matatizo yanayotokea kwa Vijana ili waendelee kuishi katika misingi ya malezi bora ya Chama cha Mapinduzi.

 “ Viongozi mliochaguliwa hivi karibuni msipofanya vizuri katika miaka mitano ijayo mtakuwa mmeharibu mfumo wa maisha yenu ya kisiasa, lakini mkitekeleza vyema majukumu  majukumu yenu itakuwa ni njia ya kupata fursa mbali mbali za kiungozi na kiutendaji ndani ya Chama na Jumuiya  ”, alisema Abdulghafar.

Aliwambia kuwa matarajio ya UVCCM ni kuona Baraza hilo ambalo ni la kwanza baada ya kumaliza  uchaguzi katika Wilaya hiyo linakuwa ni shamba darasa la kuwapata viongozi imara wenye uwezo wa kujenga hoja zenye nguvu ya kuleta mabadiliko ya kimaendeleo nchini.

Abdulighafar alisisitiza kuwa wajibu wa kila kiongozi ndani ya umoja huo ni kuongoza vizuri sambamba na kuzisoma kwa kina kanuni ya UVCCM na Katiba ya CCM ili maamuzi yoyote yatakayofanyika yaweze kuzingatia matakwa ya Kikatiba.

Aidha Kaimu Katibu Mkuu huyo, Abdulghafar umefika wakati wa kuwa na UVCCM huru yenye nguvu kiuchumi na kiutendaji hivyo viongozi wa umoja huo wanatakiwa kubuni miradi endelevu itakayosaidia vijana kujiajiri wenyewe.

“Vijana tutakapokuwa na uhakika wa kipato kupitia miradi tunayoisimamia wenyewe basi hata hao baadhi ya wanasiasa wenye fedha waliozoea kututumia kwa maslahi yao watakuwa hawana nafasi hiyo tena bali tutasimama wenyewe kutetea maslahi ya chama na jumuiya kwa ujumla.”, alieleza Kaimu Katibu Mkuu huyo.

Mapema  Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Wilaya hiyo aliyemaliza muda wake, Mussa Khamis Mzee  alijiuzulu wadhifa yake ili kupisha kikao hicho kutekeleza utaratibu wa kikanuni  wa kumdhibitisha Katibu atakayeshika nafasi hiyo kwa miaka mitano ijayo.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni