Jumatatu, 27 Novemba 2017

REJA- WATUMISHI SOMENI KATIBA CCM NA KANUNI

Na Is-haka Omar, Zanzibar.

               


WATUMISHI na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Zanzibar  wameshauriwa  kuzisoma, kuzielewa na kuzifanyia kazi kwa vitendo Katiba ya CCM ya mwaka 1977 pamoja na Kanuni zake.

Pia, wamesisitizwa kutumia miongozo hiyo ikiwemo mabadiliko ya Katiba hiyo yaliyofanywa hivi  ambayo ni nyenzo muhimu ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Chama na rasilimali watu kwa ujumla.

Akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Watumishi wa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar,  Mkufunzi kutoka Makao Makuu ya CCM Dodoma Salum Khatib Reja, amesema  Katiba ya Chama ndio chombo pekee kinachoeleza kwa upana wajibu na haki za kila mwanachama.

Amesema ukitaka kuijua CCM ni lazima uzisome na kuzielewa vizuri Katiba na Kanuni zake ni miongoni mwa vyombo vinavyosimamia ustawi wa Chama na Jumuiya zote.

Mkufunzi  Reja, ameongeza kuwa endapo watumishi hao watafuata maelekezo yaliyotolewa katika miongozo hiyo itasaidia kumaliza malalamiko na tuhuma zisisokuwa za lazima kwani kila kitu kitakuwa kimeamliwa kwa kufuata matakwa ya kikatiba.

Amesema siri ya kuimarika kwa Demokrasia ndani ya CCM ni kutokana na utamaduni wake wa kufuatwa kwa misingi ya Kikatiba badala ya matakwa binafsi ya viongozi ama Watendaji wa Chama.

“ Kila mtumishi anatakiwa kujitathimini na kutafakari kwa kina ni kwa namna gani atasaidia kuleta maendeleo ndani ya Chama ili taasisi hiyo iendelee kuwa chama bora cha kisiasa barani Afrika na Ulimwenguni kote”. Alisema.

Akitoa mada ya majukumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi Mkufunzi  Eva Degeteki, amesema miongoni mwa majukumu ya msingi ya Idara hiyo ni kuendeleza mahusiano mema na vyombo vya habari nchini ili vitangaze na kuripoti  kwa usahihi matukio na habari mbali mbali za Chama.

Kupitia mafunzo hayo, Eva amewataka watumishi hao kuendelea kujifunza itikadi na miongozo ya CCM ili kufikia malengo na shabaha za taasisi hiyo kwa ufanisi zaidi.

Akitoa neno la Shukrani Mtumishi wa CCM ,  Catherine Peter amewahi watendaji wenzake kuongeza bidii katika utekelezaji wa majukumu yao ili chama kiweze kushinda katika uchaguzi Mkuu ujao.

Kwa upande wake Muhsin Daud Suleiman,  ambaye ni miongoni mwa washiriki wa Mafunzo hayo, amesema mada zilizotolewa zimekidhi mahitaji ya watumishi hao kwani wamejifunza mambo muhimu yatakayosaidia kuongeza kasi ya kiutendaji kazini.









Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, idara ya Organizesheni CCM Zazibar , Haji Mkema Haji akifungua Mafunzo hayo yaliyofanyika Afisi Kuu CCM  Kisiwandui Unguja.

Mkufunzi wa mafunzo hayo Eva Degeteki akitoa ufafanuzi juu ya mada ya majukumu ya Idara ya Itikadi na Uenezi kwa Watumishi hao katika Mafunzo Afisi Kuu CCM, Kisiwandui Zanzibar.

Mkufunzi Ali Juma Makoa akifafanua umuhimu wa matumizi mazuri ya rasilimali fedha kwa watumishi katika mafunzo hayo.
Mkufunzi wa mafunzo hayo Filbert Mdaki Mampwepe akisisitiza suala la kujituma na ubunifu kwa watendaji hao.

Mshiriki wa mafunzo hayo Catherine Peter Nao akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wenzake.
Mshiriki wa mafunzo hayo Muhsin Daud Suleiman akizungumza kwa niaba ya Watumishi wapya katika mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi hao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni