Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini, Bi.Hudhaima
Mbarouk Tahiri akizungumza katika ziara ya Wilaya hiyo iliyofanyika katika
Ofisi ya CCM Jimbo la Kikwajuni Zanzibar.
MWENYEKITI
wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mjini, Hudhaima
Mbarouk Tahiri amewasihi vijana walioshindwa kuendelea na elimu ya juu kutokata
tamaa badala yake watumie fursa ya sekta ya ujasiriamali kujiajiri wenyewe.
Wito
huo ameutoa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa
kipindi cha miaka miwili ndani ya Jimbo la Kikwajuni Unguja, amesema vijana
wanatakiwa kuwa wabunifu katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira kwa
kujiunga na vikundi mbali mbali vinavyoanzishwa katika jimbo hilo ili
kujikwamua kimaisha.
Amesisitiza
umuhimu wa vijana wa UVCCM kujiendeleza kielimu katika fani mbali mbali kwani
kufanya hivyo kutasaidia jumuiya kuwa na vijana imara wenye ujuzi utakaosaidia
kuharakisha maendeleo ya umoja huo kwa haraka.
Pia amewashauri
vijana hao kuwa wamoja na wenye msimamo usioyumba katika kupigania maslahi ya CCM
ili iweze kushinda katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“CCM
ndio chama pekee kinachojali na kuwalea vijana katika misingi imara ya
kuwajenga kifikra, kiitikadi na kimaadili ili baadae tuwe viongozi bora tutakaoendeleza urithi
wa matunda ya maendeleo ya Waasisi wa
Mapinduzi ya Mwaka 1964 kwa vitendo.”, ameeleza Mwenyekiti huo.
Akizungumzia
tatizo la matumizi ya Dawa za kulevya, Mwenyekiti huyo wa UVCCM amesema Wilaya ya Mjini imekuwa ni miongoni mwa sehemu
zilizoathirika na janga hilo hivyo vijana wanatakiwa kujiepusha na matumizi ya
dawa hizo kwani zinaangamiza nguvu kazi ya taifa.
Naye
Katibu wa Wilaya hiyo Aboud Said Mpate , amesema lengo la ziara hiyo ni uongozi
huo kutoa shukrani kwa wanachama waliowachagua viongozi hao pamoja na kupokea
taarifa za utekelezaji wa Ilani kutoka kwa Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wa
Wilaya ya mjini ili wananchi waliowachagua waweze kujua mambo yaliyotekelezwa
kwa kipindi cha miaka miwili.
Aboud
amewataka vijana hao kuwa makini kwa kuepuka kutumiwa katika kutengeneza
makundi ya kulinda maslahi ya baadhi ya viongozi hasa wakati huu wa uchaguzi
unaoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake.
Akizungumzia
utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mwakilishi wa Jimbo hilo, Nassor Salim Jazeera
amesema viongozi wa jimbo hilo kwa kushirikiana wameanzisha miradi mbali mbali
ya maendeleo ikiwemo kuendeleza mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya milioni
300, kuanzisha vikundi vya usafi ili vijana wasiokuwa na ajira wajiajiri
wenyewe.
Mh. Jazeera amesema miradi mingine wameshauri na kushirikiana na serikali
kujenga barabara za lami mbili, ujenzi wa uwanja wa michezo wa Mao Tse Tung,
Ujenzi wa Shule ya kisasa ya Ghorofa katika Mtaa wa Mwembe shauri pamoja na
kuwasaidia akina Mama mitaji ya kuanzisha vikundi vya ujasiriamali.
Alifafanua
kuwa lengo la viongozi hao ni kuhakikisha wanamaliza kero na changamoto zote
zinazowakabili wananchi katika jimbo hilo kabla ya mwaka 2020.
Sambamba
na hayo amesifu kasi ya kiutendaji ya UVCCM katika Wilaya hiyo na kuwasihi
waendelee kushirikiana na viongozi hao bega kwa bega ili kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Ziara
hiyo ya siku nne itaendelea kufanyika
katika Majimbo yote ya UVCCM Wilaya ya Mjini Zanzibar.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni