Jumla ya shilingi milioni 35 zimetumika katika kuwasomesha zaidi ya wanafunzi 130 wasio na uwezo wanaoishi katika Jimbo la Jang’ombe kwa kipindi cha mwaka 2016-2017.
Hayo yameelezwa katika Ziara ya Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini alipotembelea katika jimbo la Jang’ombe kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa ahadi za kimaendeleo zilizoahidiwa na chama cha mapinduzi kwa wananchi.
Akilitolea ufafanuzi suala hilo mratibu wa mradi huo wa kuwasaidia wanafunzi, Ahmad Suleiman aliyewawakilisha Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Jang’ombe, amesema fedha hizo zimetolewa kwa wanafunzi waliojiunga na elimu ya juu ambao wamepatiwa asilimia 50 ya ada huku waliojiunga na vyuo vya mafunzo ya amali wamelipiwa ada kwa asilimia 100 kwa mwaka jana.
Katika hatua nyengine Suleiman amesema licha ya mwakilishi na mbunge kutumia pesa nyingi katika kulipa Ada za vyuo lakini bado kumekuwa na changamoto ya Kundi kubwa la Vijana kutomaliza mafunzo hali inayopelekea kutofikiwa kwa malengo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Mjini, Hudhaima Mbarouk Tahir amewataka Vijana wa Chama hicho kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili waweze kupata alama zitakazowawezesha kupata mkopo kiurahisi.
Amefafanua kuwa vijana watakapotumia muda mwingi katika kujiisomea wataweza kufaulu vizuri na kutimiza malengo yao waliojiwekea na kuwa msaada mkubwa kwa Chama cha Mapinduzi na Nchi kwa ujumla.
Katika hatua nyengine Mwenyekiti huyo Hudhaima amewataka Vijana wa Jimbo la Jang’ombe kuhakikisha wanaondoa tofauti zao za makundi yanayoweza kuhatarisha uhai wa jumuiya na badala yake wawe wamoja katika kulinda maslahi ya chama, jumuiya na serikali.
Ziara hiyo leo imeingia Siku ya Pili katika Wilaya ya Mjini ambapo Mwenyekiti huyo amewatembelea vijana wa jimbo la la jang’ombe kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM katika jimbo hilo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni