Jumatano, 1 Novemba 2017

UTAFITI WA MAFUTA NA GESI NI JUHUDI ZA SMZ KATIKA UTEKELEZAJI WA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM MWAKA 2015/2020.

MCHAKATO wa utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika Visiwa vya Unguja na Pemba hivi karibuni umeingia katika awamu nyengine muhimu ya kufanya Utafiti katika mwambao wa Pwani ya Zanzibar katika kitalu cha Pemba-Zanzibar, kwa kutumia meli maalum ya Kampuni ya BGP kutoka nchini China.

Hatua hiyo ya awamu ya pili ya zoezi la utafiti linaloendeshwa na kampuni ya  RAKGAS ya Ras Khaimah kutoka falme za kiarabu chini ya usimamizi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, wameanza kazi hiyo huku wakiahidi kuikamilisha kwa muda uliopangwa.

Mafuta na gesi asilia ni moja ya rasilimali zenye thamani kubwa duniani ambazo nchini mbali mbali duniani zinazomiliki na kuchimba nishati hiyo  zinatajwa kuwa imara kiuchumi.

Kwa mara ya kwanza kabisa kazi ya Utafiti wa Nishati hiyo ulifanyika Zanzibar mwaka 1952  ambao matokeo yake yalibainisha kuwepo kwa dalili za Mafuta na Gesi Asilia katika Pwani ya mwambao wa maeneo ya visiwa vya Pemba na Unguja.

Kimsingi mchakato huo ulianza miaka mingi iliyopita hivyo ni jambo ambalo bado lilikuwa katika dhamira ya utekelezaji wa awamu mbali mbali za serikali zilizopita japokuwa wakati wake ulikuwa bado haujatimia.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya awamu ya saba chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein aliahidi kusimamia zoezi la upatikanaji wa mafuta na gesi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, ikiwa ni moja ya hatua ya msingi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa wananchi wote.

Mnamo Mwezi Novemba 15 mwaka jana, Dk. Shein  alitia saini Sheria ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ili kuandaa mazingira rafiki ya kisheria yatakayotoa baraka na mamlaka ya kuanza kwa zoezi hilo.

Kutungwa kwa sheria hiyo inatokana na masharti ya kifungu cha nne Sheria ya Mafuta na Gesi Asilia 2015 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inataja kwamba shughuli za uendeshaji wa Mafuta na Gesi Asilia utafanywa Zanzibar kwa kusimamia na kuendeshwa na taasisi kwa mujibu wa Sheria za Zanzibar.

Pia kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo, Serikali ilitengeneza Sera ya Mafuta na Gesi Asilia kwa ajili ya kutoa muongozo kwa sekta hii muhimu katika uchumi wa nchi.

Katika hatua za msingi za kuharakisha mchakato wa utafutaji wa nishati, Dk. Shein mwezi machi mwaka huu alianzisha rasmi  Mamlaka ya udhibiti wa utafutaji na uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia ( ZPRA).

Akizungumzia Mhandisi wa ZPRA Mwadini Juma Khatib  anasema zoezi la Utafutaji wa nishati hiyo kwa awamu ya kwanza ulianza rasmi Machi mwaka huu,  baada ya uzinduzi uliofanywa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd uliofanywa na ndege  ya Kampuni ya Bell Geospace.

Akifafanua kuwa awamu ya pili ya utafiti huo uliozinduliwa Octobar 27, mwaka huu na Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ambao unatumia Meli Maalum kwa njia ya mtetemo ambayo kitaalamu huitwa (Seismic Survey) ni hatua ya pili baada ya hatua ya awali ya kukagua miamba iliyopo chini ya ardhi ya (FTG).

Lengo la kufanya utafti huo wa Mtetemo ni kuangalia maumbile ya miamba yenye uwezo wa kuhifadhi mafuta na gesi asilia ili wataalamu waweze kubaini maeneo ya kuchimba visima vya kutafuta nishati hiyo( Exploration Wells).

Mhandisi  Juma  wa  ZPRA,  anaeleza  kwamba  Kwa mujibu wa Kampuni ya Brunwick Zanzibar Ltd inayofanya kazi kwa niaba ya kampuni ya RAKGAS, Meli ya Utafiti kwa kutumia mtetemo ya  Kampuni  ya BGP ya China inayofanya utafiti huo  katika kitalu cha Pemba –Zanzibar , kazi inaendelea  vizuri katika maeneo husika.

Meli ya Kampuni ya Utafiti na Utafutaji wa Mafuta na Gas Asilia Zanzibar ikiwa katika bandari ya Zanzibar wakati wa uzinduzi wa Meli hiyo kuaza zoezi la Utafutaji wa Mafuta na Gas Asilia katika Visiwa vya Unguja na Pemba, Utafiti huo unafanywa na Kampuni ya
Kichina BGP Explorer.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni