Jumanne, 24 Oktoba 2017

DK.MABODI AONGOZA MAMIA YA WANANCHI KATIKA MAZIKO YA KADA WA CCM MAREHEMU HASSAN VUAI HASSAN ''NYOMBOA".

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi leo ameongoza mamia ya wanachama na wananchi katika mazishi ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa Kusini Unguja marehemu Hassan Vuai Hassan ‘’Nyomboa’’ yaliyofanyika kijijini kwao Bwejuu Wilaya ya Kusini Unguja.

Marehemu huyo ambaye pia alikuwa ni Afisa Usalama na Maadili wa CCM Wilaya ya kusini Unguja ameumwa ghafla na kufariki dunia jana akiwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja  alikopelekwa kwa ajili ya matibabu.

Akizungumza Dk. Mabodi katika mazishi hayo amesema CCM imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na imepoteza kada jasiri aliyejitolea kwa muda mrefu kulinda na kutetea maslahi ya chama hicho.

Dk. Mabodi ameeleza kwa masikitiko kuwa CCM imepata pigo kubwa baada ya kumpoteza mwanachama huyo aliyefanya kazi za chama kwa ufanisi mkubwa bila ya kuchoka na atabaki kuwa mfano wa kuigwa kwa makada wengine wanaotakiwa kumuenzi kwa kufuata nyayo zake.

Pia Dk. Mabodi alitoa salamu za pole kutoka kwa Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein aliyeelezea kusikitishwa kwake na kifo hicho na kuiomba familia ya marehemu kuwa na subra katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo.

“Marehemu Nyomboa ni mpiganiji mwenzangu tumekuwa wote toka tukiwa wadogo toka enzi za Paunia hadi tukawa wakubwa na tukaendelea kukitumikia chama, alikuwa ni mchapakazi na mtu wa watu.

Nasaha zangu sisi tuliobaki tuendelee kumuombea dua na kumuenzi kwa kufuata nyayo zake.”, alieleza kwa uzuni Dk.Mabodi.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja , Ramadhan Abdallah Ali alisema Mkoa huo umepoteza kiongozi na kada muhimu aliyekuwa ni mtu makini na asiyeyumba kwa kile anachoamini kuwa ni sahihi katika kuimarisha chama hicho kiitikadi na kisiasa.

Akisoma wasifu wa Marehemu Hassan Vuai Hassan, Kaimu Katibu wa CCM  Wilaya ya Kusini Unguja, Hafidh Hassan Mkadam amesema marehemu amefariki dunia akiwa na umri wa miaka  66 na ametumikia chama, serikali  na Jumuiya zake kwa nafasi mbali mbali za uongozi na utendaji.

Marehemu Nyomboa enzi za uhai wake ameshika nyadhifa mbali mbali zikiwemo Afisa Utumishi Afisi ndogo ya Wazazi Zanzibar, Kaimu Katibu wa CCM Wilaya ya Wete Pemba, Katibu Msaidizi wa CCM Wilaya ya Chunya, Mjumbe wa Kamati ya siasa wa CCM Wilaya na Mkoa wa Kusini Unguja, Diwani wa Wadi ya Paje.  

Katika wasifu wake marehemu ameacha vizuka wawili na watoto 13 na wajukuu 17.



Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu pahali pema pepo Amini.

Baadhi ya makada wa CCM na Wananchi wakibeba jeneza la marehemu Hassan Vuai Hassan '' Nyomboa'' kulitoa msikitini na kulipeleka katika sehemu ya makaburi ya kijiji cha Bwejuu kwa ajili ya maziko.


 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi(kulia) aliyevaa kanzu na koti jeusi na miwani na kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Zanzibar  Ndg. Vuai Ali Vuai pamoja na wananchi wengine wakiwa katika maziko ya marehemu Nyomboa.

Baadhi ya viongozi wa Chama na Serikali na Makada wengine na wananchi kwa ujumla walioudhuria mazishi ya marehemu Nyomboa wakiomba dua mara baada ya mazishi hayo.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akiwa na familia ya marehemu Hassan Vuai Hassan ''Nyomboa'' wakimwombea marehemu dua. 

   
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi akitoa mchango wa Ubani kwa  niaba ya Chama Cha Mapinduzi  katika Familia ya Marehemu Hassan Vuai Hassan.( PICHA NA AFISI KUU CCM ZANZIBAR)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni