Jumatatu, 9 Oktoba 2017

DK. MABODI ATOA NASAHA NZITO CCM W/KASKAZINI "B" UNGUJA.


CHAMA cha  Mapinduzi (CCM) Zanzibar viongozi watakaochaguliwa kupitia Uchaguzi wa ngazi ya Wilaya ya Kaskazini “B” kichama Unguja kuwa mstari wa mbele kukemea vikali vitendo vya makundi na safu za uongozi zenye nia ya kuhatarisha uhai wa CCM katika Wilaya hiyo.

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dk. Abdalla Juma Mabodi wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo wa kuwachagua  viongozi wa nafasi mbali za ngazi hiyo huko Mahonda katika ukumbi wa Ofisi ya CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema  matarajio ya CCM ni kuona viongozi  wanaochaguliwa katika uchaguzi huo wanakuwa na makundi ya kuimarisha chama na sio kukibomoa.
Dk.Mabodi alieleza kwamba msimamo wa CCM ni  kuhakikisha Katiba, kanuni na miongozo inasimamiwa  na kufuatwa ipasavyo ili kupata viongozi na makada wenye uwezo wa kuleta maendeleo yewnye tija ndani ya chama hicho kwa miaka mitano ijayo.

Aidha amewambia viongozi watakaopata nafasi ya kuchaguliwa kupitia uchaguzi huo wahakikishe wanajenga ngome imara ya kisiasa katika wilaya hiyo sambamba na  kuwashawishi wapinzani waliomo katika Wilaya hiyo kujiunga na CCM kwani ndio chama pekee kinachojali maslahi ya wananchi wote.

Amewasihi makada watakaochaguliwa kuwa viongozi kushirikiana vizuri na makada wenzao ambao hawakupata fursa ya kuchaguliwa kwa lengo la kuendeleza misingi imara ya ukomavu wa kisiasa na Demokrasia  iliyotukuka.


Hata hivyo amewapongeza wanachama hasa makada waliogombea nafasi mbali mbali kwa kutofanya kampeni za fujo, vurugu na kuchafuana hali aliyosema kuwa inaonyesha ishara njema ya kukamilika kwa uchaguzi huo bila kujitokeza mapungufu.

Aidha amesema chama hicho baada ya uchaguzi huo kinakusudia kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo  viongozi wa ngazi mbali mbali za chama ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk. Mabodi amewataka wananchi  wapuuze kauli zinazotolewa na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif za kuwa ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar  jambo ambalo haliwezi kutokea kwani Rais halali wa Zanzibar ni Dk. Ali Mohamed Shein mpaka mwaka 2020.

Katika uchaguzi huo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Wilaya , Katibu wa Siasa na Uenezi, nafasi ya mkutano Mkuu wa Mkoa , nafasi ya Mkutano Mkuu wa taifa pamoja na nafasi za Halmashauri kuu ya CCM Wilaya.


                                         MATUKIO KATIKA PICHA

Katibu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Nd. Mulla Othman Zubeir akikabidhi taarifa ya Utekelezaji kwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi huko Mahonda katika Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B"  kichama Unguja. 

 Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo Nd. Ramadhani Abdalla Shaaban kionyesha sanduku la kupigia kura kabla ya kuanza mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Wilaya hiyo.

Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kamati Kuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo akipiga kura katika uchaguzi huo.

Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya hiyo wakifuatilia kwa kina nasaha zinazotolewa na mgeni rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni