CHAMA Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kimefanya
uchaguzi wa ngazi ya Wilaya katika Mikoa ya Zanzibar ili kupata viongozi
watakaoongoza nafasi mbali mbali ndani ya ngazi hiyo kwa kipindi cha miaka
mitano.
Katika uchaguzi huo mamia ya wanachama wa chama hicho
wamejitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura kutekeleza haki yao ya
kidemokrasia kwa mujibu wa Katiba ya CCM.
Akifungua Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Kaskazini “A”
kichama Unguja, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi
katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Mahonda, amewasihi wajumbe wa
mkutano huo kutumia vyema fursa hiyo kwa kuwachagua viongozi makini na wachapa
kazi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alifafanua kwamba uchaguzi huo ni muhimu
sana kwa chama hicho kwani viongozi watakaochaguliwa watakuwa na dhamana ya
kuzitendea haki nafasi zao kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama hicho.
Alisema katika uchaguzi wa ndani wa CCM unakuwa ni wa wanachama
wote hivyo baada ya uchaguzi watakaoshinda na wale ambao kura zao hazitotosha
na wakawa hawakuchaguliwa wote wanatakiwa kushirikiana katika harakati mbali
mbali za kuleta maendeleo ya chama hicho.
Dk. Mabodi alieleza kuwa viongozi watakaochaguliwa katika
uchaguzi huo ndio jeshi la kisiasa litakaloweza kufanikisha ushindi wa CCM
katika uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2020.
Alisema katika kujenga dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya chama
hicho kimedhamiria kuondosha vitendo vyote vya rushwa, ufisadi, makundi , safu
na usaliti ili kuimarisha misingi ya demokrasia na uhuru kwa kila mwanachama
ndani ya CCM.
“ CCM Zanzibar haitoweza kuruhusu vitendo vya rushwa, makundi na
usaliti vitokee katika uchaguzi unaoendelea na mara baada ya uchaguzi kwani
lengo letu ni kukisafisha chama kiwe na viongozi waadilifu watakaosimamia
maslahi ya wananchi kwa uzalendo.”alisisitiza Dk. Mabodi.
Pamoja na hayo aliwataka viongozi watakaochaguliwa kubuni miradi
endelevu ya kiuchumi na kichama itakayoimarisha siasa katika masuala ya Itikadi
kwa kupata wanachama ambao ni makada wenye uzalendo na imani ya kuitumikia CCM
katika mazingira yoyote.
Aidha aliwasisitiza viongozi watakaochaguliwa kuwa waadilifu
wakati wa uongozi wao kwa kulinda kwa vitendo hadhi na heshima ya CCM
iliyojengwa kisiasa ndani na nje ya chama hicho.
Naye Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa, Dk.Hussein Mwinyi
akifungua mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Mjini, alisema ukomavu wa kisiasa
ulioonekana katika chaguzi za ngazi za matawi hadi majimbo uliokamilika bila
kutokea vurugu ama dalili za rushwa ndio matarajio yanayotegemewa kuonekana
katika uchaguzi wa ngazi zilizobaki.
Alisema kwa sasa CCM imeamua kujisahihisha kwa kutorudia makosa
yaliyokuwa yakitokea katika chaguzi za ndani ya chama zilizopita hivyo viongozi
watakaochaguliwa katika uchaguzi huo wafuate Katiba na kanuni za chama
cha mapinduzi.
Dk. Mwinyi alisema baada ya uchaguzi huo wanachama wa chama
hicho wanatakiwa kuendeleza mshikamano wa kuhakikisha wanajiandikisha kwa wingi
katika daftari la wapiga kura pamoja na kuongeza wanachama wapya ili
kujiimarisha kisiasa katika uchaguzi mkuu wa dola ujao.
Katika uchaguzi huo nafasi zinazowaniwa ni Mwenyekiti wa Wilaya
,Katibu wa Siasa na Uenezi, nafasi ya mkutano Mkuu wa Mkoa , nafasi ya Mkutano
Mkuu wa taifa pamoja na nafasi ya Halmashauri kuu ya CCM Wilaya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni