Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kitaendelea kuthamini kwa vitendo maarifa, mbinu na uchapakazi wa Mabalozi wa mashina katika kufanikisha harakati za maendeleo ndani ya chama hicho.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi wakati akifunga mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo juu ya Uchaguzi na Takwimu, Kazi za Mabalozi, Mageuzi katika CCM kwa Mabalozi wa CCM Jimbo la Mpendae Zanzibar, alisema mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya kuwaongezea uwezo katika utendaji wa shughuli zao za kila siku.
Alisema mabalozi hao ndio uti wa mgongo wa CCM kwani wamekuwa wakijitolea kupigania maslahi ya chama hicho katika mazingira yoyote bila ya kuchoka wala kujali changamoto za kisiasa.
Dk. Mabodi alisema matarajio ya Chama cha Mapinduzi ni kuona mabadiliko ya kiutendaji katika mashina mbali mbali ya Jimbo hilo yanayoendana na maelekezo ya taaluma waliyopewa.
“ CCM tunajivunia kuwa na makada makini na wazalendo ambao ndio nyinyi mabalozi kwani kundi lenu lipo karibu zaidi na wananchi ambao ndio wapiga kura walioiweka madarakani CCM nasi tunakuahidini kuwa hatutowaangusha.
Kukutana kwenu katika mafunzo haya ni moja ya mafanikio kwani mmebadilishana uzoefu na mikakati itakayosaidia kuimarisha chama chetu na kikapata ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.”, alieleza Dk. Mabodi.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema miongoni mwa mambo ya msingi yanayotakiwa kufanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na washiriki wa mafunzo hayo ni suala la takwimu sahihi za wanachama ambao ndio mtaji wa CCM kisiasa.
Alisema mabadiliko ya Kikatiba yaliyofanyika hivi karibuni ndani ya Chama hicho dhamira yake ni chama kurudi kwa wanachama wa ngazi za chini ambao ndio waliotoa ridhaa ya kuiweka serikali madarakani ili iweze kuwatumikia wananchi bila ubaguzi.
Hata hivyo alisisitiza kupitia Uchaguzi unaoendelea ndani ya Chama na Jumuiya zake ni lazima wapatikane viongozi wenye uwezo wa kuendelea Itikadi ya Chama na kuheshimu maadili ya uongozi kwa yanayosisitizwa kikatiba.
Hata hivyo aliwapongeza viongozi wa Jimbo hilo kwa kuandaa mafunzo hayo na kuyataka majimbo mengine kuiga utamaduni huo ili kuleta ufanisi wa pamoja ndani ya chama hicho.
Wakizungumza baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kwa wakati tofauti wameahidi kuyafanyia kazi ili kwenda sambamba na malengo ya CCM kisiasa na kiutendaji.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni