Jumatatu, 16 Oktoba 2017

DK.MABODI ASHAURI PEMBEJEO ZA KILIMO WANAZOUZIWA WAKULIMA ZIWE NA UBORA.



 
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi ameishauriserikali kuhakikisha Pembejeo za kilimo wanazouziwa wakulima zinakuwana viwango vinavyoendana na mazingira ya kilimo yaliyopo nchini.


Ushauri huo ameutoa jana wakati akizindua msimu wa kilimo cha Mpungakatika mabonde yaliyopo katika Jimbo la Bububu na vitongozi vyake ukokatika bonde la Mahakani lililopo katika kijiji cha Kizimbani Wilayaya magharibi "A".


Alisema wananchi wengi wanafanya shughuli za kilimo katika mazingira magumu hivyo ni lazima taasisi za umma zinazohusika na kuuza pembejeo za kilimo ambazo ni mbolea, dawa na mbegu kuwa makini kwa kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi vigezo vya kilimo ili kuepusha hasara kwa wakulima.


Dkt. Mabodi alitoa ufafanuzi huo baada ya Mwakilishi wa jimbo la Bububu, Mh. Masoud Abrahman Masoud kueleza kuwa katika msimu wa kilimo ulipita baadhi ya wakulima wanaolima mpunga katika mabonde ya mpunga ya jimbo hilo walipata walikosa mavuno kutokana na mpunga kukauka kwa sababu ya kutumia pembejeo mbovu zisizokuwa na viwango.


"Nitakaa na viongozi wa Wizara husika kwa lengo la kuwaeleza changamoto hiyo nao waweze kuifanyia kazi ili isiweze kujitokeza katika misimu ijayo.", alifafanua Dk. Mabodi na kuwasihi wakulima wasivunjike moyo kwani serikali yao ni makini na ina dhamira ya kuhakikisha ardhi ndogo iliyopo inatumika kwa kilimo cha kisasa.
Alieleza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 imeahidi kuisimamia serikali kuhakikisha inaweka miondombinu endelevu ya kilimo itakayosaidia Zanzibar kulima mazao ya aina mbali mbali hasa mpunga kwa lengo la kupunguza uagizishiaji wa chakula kutoka nje ya nchi.

Alisisitiza wakulima hao kuhakikisha wanaendelea kufanya maandalizi mapema ya msimu wa kilimo cha mpunga na mazao mengine ili kwenda sambamba na msimu wa mvua kwa lengo la kupata mavuno mengi.

Hata hivyo aliwasihi kuwatumia wataalamu wa kilimo ili waweze kutoa ushauri wao juu ya mbegu zinazostahili kupandwa kwa mujibu wa maeneo husika ya kilimo.

Aliwapongeza viongozi wa Jimbo la Bububu ambao ni Mbunge, Mwakilishi na Madiwani kwa ushirikiano wao unaozaa matunda ya kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020  kwa vitendo kwa kuanzisha mradi wa kilimo cha mpunga unaowanufaisha wakulima wengi wa jimbo hilo.

Akizungumzia uchaguzi unaondelea ndani ya CCM Dk.Mabodi alisema msimamo wa chama hicho ni kuhakikisha viongozi wanaochaguliwa wanakuwa ni viongozi safi kimatendo, kimaadili na wanaokubalika katika jamii na wenye uwezo wa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa dola wa  mwaka 2020.

" Ajenda ya wapinzani ni kuzungumzia uchaguzi uliopita na kuzua na kuaminishana mambo ambayo hayawezekani kutekelezeka lakini CCM kazi yetu kubwa ni kuwapelekea maendeleo wanachama wetu popote walipo nasi tunawafikia", alisema Dk. Mabodi.

Sambamba na hayo Dk.Mabodi aliahidi kuchangia nusu ya fedha za kununua tirekta ndogo aina ya Powertiller ili iweze kuwasaidia wakulima hao katika shughuli za kilimo.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Mh. Mwantakaje Haji Juma alisema mradi huo wa kilimo cha mpunga umeendeshwa kwa awamu tatu na kuwapatia wananchi mafanikio makubwa ya chakula na awamu ya sasa jumla ya shilingi milioni 16 zinatarajia kutumika fedha zitakazotolewa na mbunge na mwakilishi wa jimbo hilo.

Akisoma risala kwa niaba ya wakulima wa jimbo hilo, Bw. Saleh Said Njonjo alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na kupunguziwa bei ya pembejeo za kilimo pamoja na kupunguziwa bei ya kulimiwa na matrekita ya serikali katika mabonde yao.


Hata hivyo alisema kuwa jumla ya wakulima 723 wa jimbo hilo na maeneo jirani watanufaika na mradi huo wa kilimo cha mpunga katika mabonde ya Mahekani, Tomokani, Mkanyageni, Mkuruwinda, Ndagoni, Mbuyuni Dole, Kichakani Bumbwisudi, Shamba ndogo, chemchem, kipanga na saraya.

Kwa upande wake mkulima wa bonde la mahekani, Bw. Abdalla Haji Abdalla amesifu juhudi za viongozi wa jimbo la Bububu kwa kuwajali wakulima wa jimbo hilo na kuelezea kuwa yeye ni mmoja kati ya watu walionufaika na mradi wa kilimo cha mbunga kwa awamu mbili zilizopita.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni