Jumapili, 10 Mei 2015

DKT. SHEIN AWAONGOZA WANA CCM MAZIKO YA MAKADA WA CHAMA HICHO




MAKAMU Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, leo (mei 10, 2015) amewaongoza mamia ya Wana CCM waliohudhuria maziko ya Makada wawili kati ya watu wa Chama Cha Mapinduzi waliofariki dunia kutokana na ajili ya gari.

Makada hao waliozikwa katika makaburi  ya Mwanakwerekwe ni pamoja na Mwanaidi  Zamir Haji (28), mkazi wa Magogoni na Mwanahawa Haji Machano (50), mkazi wa Mkele, Wilaya ya Mjini. 

Aidha, Mjumbe wa Kamati Kuu na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, aliwaongoza wananchi wa Jimbo la Mkwajuni waliohudhuria maziko ya kada mwengine wa CCM Munira Abdullah (16), aliyezikwa Kijijini kwao Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini “A”.

Wana CCM hao watatu walifikwa  na umati na wengine saba kujeruhiwa kufuatia gari (basi) walilokuwa wakisafiria kutoka Nungwi kuja Mjini kupasuka mpira wa mbele na kupinduka baada ya kugonga gari la ng’ombe, katika maeneo ya Mto wa Pwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Makada waliolazwa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, ni pamoja na Maua Haji Khamis (54), Salhiya Sheha Khamis (26) na Sawadi Haji Khamis (38), wote wakazi wa Kwamtipura, Mjini Unguja. 

Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa mshituko, kuhuzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya makada wake hao, kwani walikuwa mstari wa mbele katika kikilinda, kikihifadhi, kukipigania na kukitetea kwa nguvu zao zote Chama hicho. Aidha, wanamuomba  Mwenyezi Mungu, Muumba Mbingu na  Ardhi, awape nafuu majeruhi wote waliolazwa hospitali, ili wapone haraka na kuungana na wananchi wengine  katika ujenzi wa taifa.

“Kwa niaba ya Viongozi na Wanachama wa CCM, na kwa niaba yangu binafsi, nachukua nafasi hii kuwapa mkono wa pole wana familia, ndugu na jamaa wote wa marehemu hao, kufuati  vifo hivyo”. Alisema Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar Ndugu Vuai Ali Vuai, alipokuwa akiwafariji moja ya wanafamilia ya maiti hao.

Chama Cha Mapinduzi kimesema kinatambua machungu waliyonayo wanafamilia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu hao, lakini kinawaomba kuwa na moyo wa subra na kinaungana nao, katika kipindi hiki kigumu cha maombolezi ya wapendwa wao hao.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni