Jumapili, 10 Mei 2015

CCM ina uhodari mkubwa wa kukabili...Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa kina uhodari mkubwa wa kukabili changamoto na kuheshimu mageuezi ya kifikra, kidemokrasia, kiuchumi  na kisiasa.

Tamko hilo limetamkwa na Mwakilishi wa Jimbo la Mwembemakumbi Machano Othman Said, wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Tawi la Kinyasini, Wilaya ya Kaskazini ‘A’, Unguja.

Mwakilishi huyo, ambaye ni Waziri Asiyekuwa na Wizara Maalum wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) amesema historia ya CCM kabla ya mwaka 1977 imeonyesha jinsi chama hicho kilivyopita na kufuzu katika vipindi vingi vya mpito bila ya kuyumba, kubabaika wala kutetereka.

Amesema mwaka 1977 vyama vya ASP na TANU vilifanya mageuzi makubwa ya kisasa kwa kuunganisha nguvu za kisiasa, mwaka 1992 nchi ikatoka katika mfumo wa chama kimoja hadi vyama vingi na sera za CCM kiuchumi zikabadilika toka uchumi hodhi hadi soko huria.

Akizungumnzia  hali ya kisiasa Zanzibar na mivutano  yake mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995,2000 na 2005, amesema CCM iliona umuhimu wa kuwauliza wananchi ili kuridhia au kutoridhia  kuendelea na mfumo wa anayeshinda kuchukua vyote au kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kuhusu Katiba Inayopendekezwa, Mhe. Machano amesisitiza haja kwa wana CCM na wananchi wapenda amani na utulivu wa Wilaya hiyo (Kaskazini ‘A’) kutofanya makosa na badala yake waipigie kura ya ndio Katiba hiyo wakati utakapofika.

Ametoa wito kwa wana CCM kutobabaishwa na kauli za wapinzani  bali waelekeze nguvu zaidi katika kuisoma na kuifahamu vyema Katiba Pendekezwa, kabla ya kuchukua maamuzi sahihi kwa maslahi yao, vizazi vya leo na vya baadae.   

Alitumia kikao hicho kukabidhi Seti ya TV pamoja na king’amuzi kwa uongozi wa Maskani ya Chama Cha Mapinduzi ‘Bado Tungalipo’ ya Tawi hilo la Kinyasini Wilayani humo.

Akitoa neno la shukrani, Diwani wa Wadi ya Kinyasini Khamis Amour  Ame, amefarajika na msaada huo, ambao ulikuwa ukitakiwa sana na vijana hao wa Maskani  na kuahidi kuahidi kuitumia kama ilivyokusudiwa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni