Jumatatu, 3 Oktoba 2016

WANACCM WATAKIWA KUWANIA NAFASI ZA UONGOZI

WAFUASI wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “B” kichama wameshauriwa  kujiandaa kisaikolojia  kuwania nafasi za uongozi katika Uchaguzi ujao wa CCM  ili kupata viongozi bora  watakaokuwa na uwezo na weledi wa kiutendaji.



Akizungumza kwa nyakati tofauti  Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, idara ya Itikadi na Uenezi Zanzibar,  Waride Bakar Jabu katika ziara ya kuimarisha Chama huko  katika  Matawi ya Bubwini Mafufuni na Donge Kitaruni.


Alisema  maandalizi yakifanyika mapema kwa kutoa taarifa mbali mbali kwa watu wenye nia na sifa za kugombea uongozi zinazokubalika ndani ya CCM itasaidia kuwapata viongozi wazuri na waliokomaa kisiasa.


Alieleza kwamba suala la kujiandaa kuwa kiongozi ndani ya Chama hicho linatakiwa kwenda sambamba na kujitathimini hali ya kisiasa iliyopo ndani na nje ya chama hicho kwa lengo la kupata fikra mpya zitakazoiwezesha CCM kushinda katika uchaguzi Mkuu wa 2020.


“Kwanza CCM inawapongeza Wilaya ya Kaskazini “B” kupitia majimbo yenu mmefanya kazi nzuri katika Chaguzi zote zilizopita chama kimeweza kushinda kwa ngazi mbali mbali na kushika Dola.


Pia nakukumbusheni viongozi muanze  mapema kutoa taarifa kwa wanachama ili wapate muda mzuri wa kujiandaa na uchaguzi huo wa chama ili kupata viongozi wenye uwezo kiutendaji na kukabiliana na changamoto za kisiasa zilizopo Zanzibar, na kuepuka malalamiko yasiyokuwa ya lazima.”, alifafanua Waride.


Aliwasihi viongozi wa Majimbo wakiwemo wabunge , wawakilishi na madiwani kushirikiana na viongozi wa Chama katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 ili kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili wananchi.


Aliwaagiza viongozi wa matawi ndani ya wilaya hiyo kufanya vikao vya mara kwa mara ili kujadili na kubuni njia mbadala ya kuongeza wanachama wapya ndani ya chama ambao ndio wapiga kura halali katika Uchaguzi Mkuu ujao.


Naye Katibu wa Kamati Maalum Idara ya Ogarnazesheni ya CCM Zanzibar, Haji Mkema alisema lengo lla ziara hiyo ni kuwapongeza wanachama wa chama hicho na wananchi kwa ujumla kwa kuichagua CCM kwa kura nyingi na hatimaye ikaongoza dola.


Aliwambia Makatibu wa Chama wa ngazi mbali mbali ndani ya Wilaya hiyo kujenga utamaduni wa kuandaa takwimu sahihi za wanachama kwa lengo la kujua ni wanachama wangapi wamepungua na  wameongezeka.


Mkema alisema wafuasi wa Chama hicho wanatakiwa kufanya kazi za kuimarisha CCM , lakini pia watumie fursa zinazowazunguka zikiwemo kilimo cha biashara na Chakula  kujenga uchumi wao.


“ Tufanye siasa kwa kuimarisha chama chetu, lakini pia tunatakiwa kujenga uchumi wetu kwa kutumia fursa zinazotuzunguka zikiwemo kilimo cha biashara kwani ardhi yetu ya Donge ina historia ya rutuba kwa mazao mbali mbali hasa Karafuu.”, alishauri Mkema.


Hata hivyo aliwataka wanachama hao kujiunga na Jumuiya mbali mbali za CCM hasa za wanawake na vijana ili waweze kunufaika na fursa mbali mbali zinazopatikana kupitia jumuiya hizo na kuweza kujikwamua kiuchumi.


Kwa upande wa wanachama wa chama hicho waliiomba CCM kuendelea kuishauri serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana wanaoishi maeneo ya vijijini.


Aidha ameiomba serikali kudhibiti  vitendo vya uhamiaji holela ndani ya Wilaya hiyo kwani unasababisha kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na kuibuka kwa tabia zisizofaa katika jamii.




























Hakuna maoni:

Chapisha Maoni