Jumatano, 13 Desemba 2017

JUKUMU LETU UWT NI KUHAKIKISHA 2020 CCM INABAKIA MADARAKANI


NA EMMANUEL MOHAMED, ZANZIBAR

MAKAMU Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi(UWT), Zanzibar,Thuwaiba Edinton Kisasi,ameitaka jumuia hiyo kuvunja makundi yaliojitokeza wakati wa uchaguzi wa nafasi mbalimbali za umoja huo na kwamba jukumu liloko mbele ni kuhakikisha CCM inashinda mwaka 2020.

Amesema uchaguzi si uhasama hivyo tofauti za makundi katika kipindi hicho kimemalizika na ni wakati wa kukipigania chama.

Hayo aliyasema jana, wakati akikaribishwa ofisini kwake ilioko Kisiwandui, mjini Unguja ambapo alisema ni kawaida ya CCM ikifika kipindi cha uchaguzi wa ndani kuwepo kwa makundi ya kumtaka mgombea fulani lakini ukiisha wana-CCM wanakuwa wa moja.

Katika maelezo yake Makamu Mwenyekiti huyo, aliongeza kuwa UWT inapaswa kuondoa tofauti zake hizo na kwamba kazi ilioko sasa ni kuunganisha wanawake na kuwaongeza idadi mpya ya wanachama wapya ndani ya jumuia hiyo na CCM.

"Tuondoe tofauti zetu ambazo zilikuwepo kwenye uchaguzi huu na tujengee jumuia hii uwezo mkubwa pamoja na chama chetu na niaomba nisisitize kufanya kazi kwa kasi zaidi,"alisema.

Makamu huyo Mwenyekiti aliitaka jumuia hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na kutokukiuka miongozo ya chama hivyo ni wakati muafaka wa kuimarisha UWT ili kuisaidia CCM kushinda mwaka 2020.
     
Thuwaiba aliwataka wanajumuia hiyo ya UWT kufanya kazi kwa kasi zaidi kwa ajili ya kuhakikishia ushindi mwaka 2020 na kwamba kutokana na kuwepo kwa demokrasia imara ndani ya CCM wapinzani wameanza kurejea ndani ya chama.

"Msiwabeze wapinzani ambao wanatoka kwao huko kwenye vyama vya siasa ambavyo havina misingi ya demokrasia kutokana na kuwa wameona CCM ina miongozo yake hivyo hatuna makundi tofauti za ovyo ovyo wana-CCM ni wamoja na lengo ni kukipigania chama ili kuendelea kushika dola,"alisema Makamu Mwenyekiti.

Mbali na hilo, Makamu Mwenyekiti huyo aliwapokea wanachama wapya 94 kutoka vyama vya upinzani,ambapo aliwakabidhi kadi za CCM na kula kiapo cha uadilifu cha chama.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UWT,Zanzibar, Salama Aboud Talib, alimuomba Mwenyekiti huyo kushirikiana na watendaji wa UWT kwa ajili ya kufanikisha ushindi wa mwaka 2020 katika uchaguzi ujao.

Aliongeza kuwa jumuia hiyo haiwezi kufanikiwa bila ya kuwepo na ushirikiano na watendaji wa ngazi zote kuanzia wilaya hadi mikoa hivyo ni wakati wa kufanya kazi kwa kushirikiana.

Naibu Katibu huyo wa UWT, alisema jumuia hiyo inapaswa kufanya kazi kubwa ya kulea kama ilivyo jukumu lake katika taratibu zake za chama hivyo ni wakati wake.

"Nikuhakikishie kuwa watendaji wote wa UWT ni wazuri na uwakika watakupa ushirikiano mkubwa kwenye kufanya kazi licha ya kuwepo kwa watendaji wapya hivyo kupitia semina na mafunzo yatawawezesha kujenga siasa visiwani humu,"alisema.









Hakuna maoni:

Chapisha Maoni