Jumanne, 5 Desemba 2017

BALOZI SEIF ALI IDD-WAPINZANI WASALIMU AMRI

 Na Is-haka Omar,Picha na Abeid Machano Kh - Zanzibar.

MJUMBE wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Balozi Seif Ali Idd amesema wapinzani wa vyama vya siasa wameanza kusalimu  amri kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana utendaji na  usimamizi wa Mwenyekiti wake Dk.John Magufuli  katika kusimamia sera na ilani ya chama.

Amesema kwa sasa wapinzani hawana ajenda wala  hoja na kwamba yote waliokuwa wanayasema CCM inaisimamia vyema ikiwemo kupinga suala la ufisadi na kulinda  rasilimali za taifa.

Hayo aliyasema jana katika mkutano mkuu wa uchaguzi wa mkoa wa Kaskazini, Unguja,ambapo aliongeza kuwa hadi sasa imejionesha dhahiri baada ya baadhi ya  wapinzani kurejea CCM huku wakidai hawana sababu ya kupingana na chama kutokana na utendaji mzuri wa Mwenyekiti Dk.Magufuli.

Katika maelezo yake Makamu huyo wa pili wa Rais alisema kutokana na kazi nzuri inayoendelewa kufanywa na CCM tayari dalili za ushindi katika uchaguzi wa mwaka 2020 umeanza kuonekana mapema.

"Wote mashahidi kuwa wapinzani wamejisalimisha CCM akiwemo Mwenyekiti wa Baraza la vijana wa CHADEMA, na wengineo na jambo kubwa limeanza kujionesha katika ushindi wa uchaguzi mdogo wa kata 43 ambapo hadi kwenye maeneo ya wapinzani wamenyanganywa hii ni dalili nzuri sana kwa CCM,"alisema

Balozi Seif alisema anampongeza Mwenyekiti wa Chama Dk.Magufuli kutokana na usimamizi wake makini wa sera na ilani  ya CCM na hiyo ndio sababu wapinzani wameanza kusalimu amri.

Alisema kutokana na sababu hiyo ya utendaji makini Dk.Magufuli wapinzani wamenyanganywa hoja zao za kupinga ubadhirifu wa rasilimali za nchi, rushwa, ufisadi na ukasanyaji wa kodi.

     
"kama uchaguzi mdogo huu ambao CCM imeshinda kata 42 kati ya  43 ambapo wapinzani wameambulia moja ni dhahiri kuwa mchezo huu utaendelea vilevile katika uchaguzi wa mwaka 2020,"aliongeza

Mbali na hilo, Balozi Idd alisema katika uchaguzi wa mwaka  2020 kwa upande wa Zanzibar CCM itahakikisha inapora  na kunyanganya majimbo yote ya wapinzani kutokana na kuwa hawana hoja wala ajenda tena.

Aliwasisitiza wajumbe wa mkutano huo mkuu wa uchaguzi kuchagua viongozi ambao watahakikisha wanachukua
majimbo ya wapinzani katika uchaguzi wa mwaka 2020 pia kuimarisha chama kwa mkoa wa Kaskazini.

"Viongozi ambao watachaguliwa leo ni wale ambao watakuwa na sifa za uongozi na watakaobuni miradi mbalimbali  itakayosaidia chama kutokuwa omba omba kwenye mipango yake ya Mkoa,"alisema.

Pia, Makamu huyo wa pili wa Rais, aliwataka viongozi hao ambao watachaguliwa kuendeleza na kusimamia sera na ilani ya Chama ya kupiga vita ubadhirifu wa rasilimali na wafanye kazi usiku na mchana na kwamba wavunje makundi kutokana na kuwa yanaumiza chama.

Alisema viongozi watakaochaguliwa ni lazima wavunje makundi yote mara baada ya uchaguzi huo na wabaki na kundi moja litakalosimamia maslahi ya wanachama.

Balozi Seif Ali Iddi ambaye pia ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, alisema wanachama wababaishaji na wasioaminika hawafai kupewa nafasi za uongozi kwani watahatarisha uhai wa Chama Cha Mapinduzi.

"Msichague viongozi ambao mchana CCM, na usiku wapo katika vyama vingine vinavyokesha vikipanga mbinu za kutuondosha madarakani".alisisitiza Balozi.

Aliwambia wanachama wanachama watakaoshindwa kupata nafasi za uongozi kupitia uchaguzi huo wasivunjike moyo bali wajihesabu kuwa kura zao hazikutosha na washirikiane na viongozi walioshinda kukijenga Chama.

Aliwakumbusha majukumu ya msingi viongozi watakaochaguliwa kuwa wanatakiwa kuhakikisha chama kuanzia ngazi za mashina hadi mikoa wanafanya vikao vya kikanuni kwa mujibu wa Katiba ya CCM, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji katika ngazi hizo.

  

Baadhi ya wajumbe na viongozi wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakiimba nyimbo za chama ikiwa ni miongoni mwa mapokezi ya mgeni rasmi.

Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM Taifa, Balozi Seif Ali Iddi (kushoto) Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi (katikati) Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Haji Omar Kheir.

 Baadhi ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Balozi Seif Ali Iddi akiwahutubia wanachama, viongozi na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi huo, Seif Shaaban akitoa ufafanuzi na taratibu za uchaguzi kwa wajumbe wa Mkutano.



Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Balozi Seif Ali Iddi, akipiga kura za kuwachagua viongozi  wa CCM watakaoongoza miaka mitano ijayo.

 Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini "B" Issa Juma Ali(kushoto) Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Zanzibar  Mzee Ali Ameir Mohamed wakiwa katika Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni