Alhamisi, 28 Desemba 2017

DK.MABODI-ATOA AHADI YA KUSHIRIKIANA NA UVCCM

VIONGOZI mbali mbali wa UVCCM pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Mabodi wakiomba dua katika Kaburi la Marehemu Mzee Abeid Amani Karume lililopo katika  eneo la Afisi Kuu ya CCM Zanzibar.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  Dk. Abdalla Juma Saadalla(Mabodi)  amewahakikishia  Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) kuwa ataendelea kushirikiana nao katika masuala  mbali mbali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Ahadi hiyo ameitoa wakati akizungumza na viongozi wa UVCCM Taifa wakiongozwa na Mwenyekiti Kheir James na Makamu Mwenyekiti Tabia Maulid Mwita, waliofika  Afisi Kuu ya CCM Zanzibar kwa ajili ya kutembelea  na kuomba dua katika  kaburi  la aliyekuwa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Aman Karume .

Dk. Mabodi aliwambia viongozi hao kwamba kumbukumbu  na historia ya Marehemu Mzee Abeid karume inatakiwa kulindwa na vijana wa CCM ambao wao ndio viongozi wa sasa na baadae wenye dhamana ya kulinda  serikali na Chama visichukuliwe na wapinzani.

Naibu Katibu Mkuu huo amemtaja  Marehemu Mzee  Abeid Karume kuwa alikuwa ni kiongozi  wa Mapinduzi mwenyekiti  aliyekuwa na azna kubwa ya busara na falsafa pana ya masuala ya uongozi na ubunifu ndani na nje ya ASP na Serikali kwa ujumla.

Amesema  Afisi Kuu ya CCM Zanzibar inayoongozwa na  Makamu Mwenyekiti Dk.Ali Mohamed Shein itatoa ushirikiano kwa UVCCM pamoja na jumuiya na taasisi zote za kisiasa na kiserikali ili wananchi waendelee kupata huduma bora za kijamii, kichumi na kisiasa.

Pia, ameueleza msafara huo wa viongozi wa UVCCM waliofika Zanzibar kwa mara ya kwanza toka wachaguliwe kupitia Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja huo Taifa, kwamba maendeleo yaliyopatikana visiwani Zanzibar yanatokana na juhudi za CCM kuisimamia Serikali itekeleze  Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020.

“Kwanza karibuni sana Kisiwandui ambapo ndio sehemu pekee yenye historia na  Ofisi za waasisi wetu wa Afro Shiraz Party (ASP), walioanzisha harakati za ukombozi wa Waafrika wa visiwa vya Zanzibar na hatimaye  Januari 12, 1964 wakaung’oa utawala wa kisultani na kusimamisha  Dola huru iliyojali maisha na utu wa watu wote.

Nyinyi vijana ni azna kubwa kwa chama chetu hivyo fanyeni kazi kwa ufanisi ili kulinda heshima na dhamana mnazopewa kwa lengo la kuwanufaisha  vijana wenzenu ambao kwa njia moja ama nyingine hawajajaliwa kama zenu”, alisema Dk.Mabodi.

Naye Mwenyekiti wa UVCCM  Taifa , Kheir James  amekipongeza Chama cha Mapinduzi Zanzibar kwa juhudi zake za kuimarisha taasisi hiyo ya kisiasa licha ya kuwepo na changamoto za kisiasa zinazosababishwa na wapinzani.

Mwenyekiti  Kheir amesema  yupo tayari kufanya kazi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi na Serikali kwa ujumla ili changamoto mbali mbali zinazowakabili vijana ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na taasisi hizo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni