MWENYEKITI Mstaafu wa CCM Taifa, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete |
NA IS-HAKA
OMAR,DODOMA.
RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amesema hakuna shule ya urais na
uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Amesema hayo kwenye mkutano mkuu wa CCM mjini Dodoma. Kikwete
mbaye ni mwenyekiti mstaafu wa CCM akiwa wa kwanza kutoa salamu aliueleza
mkutano huo kuwa hakuna anayesomea uenyekiti au urais ila mhusika anasoma akiwa
ndani.
Amesema alitambua fika kuwa Rais John Magufuli ndiye mtu
anayefaa kwenye nafasi hiyo licha ya kupata maswali kutoka kwa watu
walioonyesha wasiwasi.
Amesema, “Nilimtetea Magufuli watu walihoji hajawahi kuwa
hata mjumbe wa shina iweje ghafla aje kuwa mwenyekiti wa chama.
Nikawaambia ataweza kwani haiitaji shule.” “Urais na
uenyekiti hauna kwenda kusoma, unasomea humohumo ndani ukishapata ile dhamana,
bora akili yako iwe nzuri ikiwa mbovu ndiyo inaweza kuleta shida, lakini huyu
wa kwetu yupo vizuri tena kaongezea na PhD, tuna kila sababu ya kushukuru
tumepata kiongozi mzuri,” amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka miwili, Magufuli amefanya
mambo makubwa yanayoleta matumaini na ameonyesha ujasiri wa hali ya juu.
“Mpaka sasa ‘big up’
mtani wangu. Kazi hii ngumu sana, sababu mimi nimeifanya. Katika kazi ngumu
duniani hii ndiyo kiboko. Uzuri na ubaya wa kazi hii ina upweke mkubwa,”
amesema.
Kuhusu malalamiko ya hali ngumu ya maisha Kikwete amesema,
“Kuweni na subira, viongozi wetu makini wanatambua matatizo yanayowakabili
wananchi na ninaamini wanayatafutia ufumbuzi.” Mwenyekiti huyo mstaafu wa CCM
aligusia mwenendo wa chama hicho na kueleza kuwa wastaafu wanafarijika hali ya
chama ikiwa shwari.
“Sisi tulistaafu faraja yetu kubwa ni kuona chama chetu
kinaendelea kuwa imara. Tukija kwenye mikutano na watu wanafurahi na sisi mioyo
inakuwa baridi.
Lakini tukisikia mivurugano kwenye chama tunaweza pata
magonjwa ya moyo,” amesema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni