NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.
BAADHI ya Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tisa
wa Umoja wa Wazazi CCM Taifa, wamesema wakati umefika wa Umoja huo kuwa shamba
darasa la Jumuiya zingine kujifunza kwao mambo mema ya kiutendaji, uadilifu
pamoja na uzalendo.
Wakizungumza kwa wakati tofauti na
mwandishi wa habari hizi katika mkutano wa Mkuu wa Tisa wa Jumuiya hiyo,
wamesema umoja huo umebeba rika la watu wenye umri na mazingatio ya utu uzima
yaliyojaa busara na hekima.
Kwa mtazamo huo, wameeleza kuwa kila jambo
linalofanywa nadani ya umoja huo kwa sasa liwe ni nukta ya kujifunza na
kuwaelekeza mambo mema wanachama wa Jumuiya zingine ndani ya Chama cha
Mapinduzi.
Akizungumza Mwenyekiti wa Umoja huo Mkoa
wa Mara Ekwabi Denis Michael, alisema maendeleo ya taasisi hiyo hayawezi
kuletwa na mtu mmoja bali yatapatikana kwa ushirikiano baina ya viongozi na
wanachama wote.
Amewasihi viongozi wenzake kwa ngazi mbali
mbali kujipangia mipango mikakati ya utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku
ili jumuiya hiyo iweze kuondokana na utendaji wa kimazoea kwa baadhi ya
viongozi na watendaji.
Naye Katibu wa Umoja huo Mkoa wa
Shinyanga, Masanja Salu amesema viongozi wote bila ya kujali vyeo walivyonavyo
wanatakiwa kushuka ngazi za chini kufahamu changamoto na kuzitafutia ufumbuzi
hatua itakayochangia kupatikana kwa wanachama wapya wa kujiunga na umoja huo na
Chama kwa ujumla.
Hata hivyo aliongeza kwamba rasilimali
zinazomilikiwa na umoja huo katika Mikoa mbali mbali endapo ikisimamiwa vizuri
na kitaalam itaingiza mapato ya kumaliza changamoto za ukata wa fedha kwa
watumishi wa taasisi hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni