Jumanne, 19 Desemba 2017

DK.SALIM-ASEMA CCM NI CHAMA BORA DUNIANI

 WAZIRI Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim
NA IS-HAKA OMAR, DODOMA.

WAZIRI Mkuu mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim amesema umuhimu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuendelea kuwa imara kunatokana na chama hicho kuwa chama tegemeo si tu katika bara la Afrika, bali duniani kote.

Dk Salim alisema hayo wakati akitoa salamu zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa chama hicho, uliofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, mjini Dodoma jana. 

Waziri Mkuu mstaafu huyo ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Jumuiya ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa (UN), alisema macho na masikio ya Afrika na Dunia kwa sasa ni kwa CCM.

Alisema pamoja na kupita katika hatua mbalimbali, CCM kimeendelea kuwa chama cha mfano katika kudumisha demokrasia na kukifanya kuwa chama cha mfano miongoni mwa vyama vya Ukombozi katika Bara la Afrika vinavyoendelea kuwa tegemeo.

“Ni lazima viongozi na wachama wote wa CCM walitambue hilo, kuwa uimara wa CCM una maana kubwa si tu kwa Tanzania bali kwa Bara letu la Afrika na Dunia yote. Macho ya wakubwa wote hivi sasa ni kwa Chama cha Mapinduzi,” alisema Dk Salim.

Dk Salim alikuwa miongoni mwa viongozi wastaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali, walioeleza kuridhishwa na uongozi na utendaji kazi wa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais John Magufuli katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.

Naye Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliwaambia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete mjini Dodoma jana kuwa viongozi wastaafu, wamefarijika na hatua ya uongozi wa Taifa wa CCM, kuwaalika viongozi hao na wamefarijika kuona chama hicho kikiendelea kufanya mikutano yake katika hali ya amani na utulivu.

Alisema kazi iliyofanywa na Rais Magufuli katika kipindi cha miaka miwili, lakini pia kazi ya uenyekiti aliyoifanya katika kipindi cha mwaka mmoja ni kubwa na imeweza kudhihirisha uwezo wa chama hicho katika kuiongoza nchi.

Alisema hata hivyo pamoja na mambo mengi yanayofanywa, yapo mengine ambayo bado hayajafanyika na kuwataka wananchi kuwa na subira wakati mambo hayo yanafanyiwa kazi.

“Mambo ya kufanya katika nchi ni mengi, hayawezi kuisha kwa miaka miwili, maana huko mitaani tunasikia ‘mzee vyuma vimekaza’, kuweni na subira, viongozi wetu makini wanatambua matatizo ya wananchi, wanayatafutia ufumbuzi, huwezi kumaliza kila kitu na nchi ikawa safi kwa miaka miwili tu.

“Tumesikia hotuba ya viongozi wetu, ya Mwenyekiti (Magufuli) na Katibu (Abdulrahman Kinana) ni hotuba nzuri sana, Mkutano Mkuu wa CCM kila unapofanyika unajenga ari mpya, unaleta matumaini mapya kuhusu kujenga chama chetu kwa viongozi na wanachama, matumaini haya hayaji bila maono ya viongozi wetu.

“Tulipokuwa kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu, kazi moja niliyokuwa nayo kama Mwenyekiti ilikuwa ni kutetea kuwa Magufuli anafaa kuwa kiongozi wetu, Kulikuwa na kelele nyingi mara ‘oooh mzee hajawahi kuwa hata balozi wa nyumba kumi, balozi wa shina, inakuaje anatoka tu huko na kuwa Mwenyekiti wa Taifa, itawezekana kweli’, nikasema inawezekana.

“Bahati mbaya au nzuri, kazi ya uenyekiti na urais haina shule ya kwenda kusoma, unasomea humo humo ndani ukishapata hiyo dhamana, bora akili yako iwe nzuri. Kwa bahati nzuri Rais wetu ana Shahada ya kwanza, ya pili na ya tatu.

“Sasa amekamilika, anaeleza mambo ya nchi kwa ufasaha, anaeleza mtazamo wake kuhusu nchi, anataja mambo ya msingi ambayo chama chetu kinapaswa kifanye, kilichobakia ni kumjazia kura ili kumpa nguvu,” alisema Kikwete.

Kikwete alisema hali ya chama hicho ni shwari, tulivu na kwamba viongozi hao wamefurahi kuona kinaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu. 

Viongozi wengine waliopata nafasi ya kutoa salamu katika Mkutano Mkuu huo ni Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu mstaafu John Malecela na Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda ambao wote walimpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kuongoza nchi na chama hicho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni