NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdalla Juma Mabodi. |
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Dk. Abdulla Juma
Mabodi amewataka viongozi wa ngazi mbali mbali waliochaguliwa kuwatumikia
wanachama kujiandaa kisaikolojia kufanya
kazi kwa weledi na ubunifu kwa lengo la kulinda hadhi na heshima ya chama
hicho.
Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza katika mahojiano maalum, amesema
njia pekee ya viongozi waliochaguliwa ndani ya chama kuanzia ngazi za mashina
hadi taifa kulipa mema kwa wanachama wao ni kufanya kazi kwa bidii ili kuleta
maendeleo endeleo kwa taasisi hiyo na kwa mwanachama mmoja mmoja.
Amesema baada ya Chama cha Mapinduzi kusajili rasmi jeshi
lake la kisiasa kupitia uchaguzi huru na wa haki uliozingatia vigezo vyote vya
kidemokrasia na Kikatiba , kwa sasa kazi iliyobaki ni kuanza mapambano
kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika chaguzi za serikali za mitaa
mwaka 2019 pamoja na uchaguzi Mkuu ujao.
“Chama chetu kimepata viongozi wa ngazi mbali mbali ambao tumechaguliwa
na wanachama wetu ili tuwatumikie kwa miaka mitano ijayo hivyo mimi nikiwa
miongoni mwa waliochaguliwa nakuombeni tutumie uwezo na maarifa yetu kuleta
mabadiliko ya kimaendeleo ndani ya chama.
Pia tutafakari kwa kina ni mambo gani ya msingi tunayotakiwa
kuyafanyia kazi kabla ya 2020, ili tuyaweke katika mipango mikakati yetu kwa
lengo la kuwahudumia wananchi wote.”, alisema Dk. Mabodi.
Aliwambia viongozi hao kwamba watambue kuwa baada ya kupewa
jukumu la uongozi wanatakiwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020 huku wakiongeza wanachama wapya ndani ya taasisi hiyo.
Alisema viongozi hao
licha ya kuwa na majukumu ya kisiasa bado wanatakiwa kuwa na uthubutu wa kubuni
miradi mbali mbali ya kiuchumi ili itoe ajira kwa wananchi ambao ndio mtaji wa
kudumu wa Chama cha Mapinduzi.
Aidha amewashukru wanachama wa chama hicho hasa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa
CCM Taifa kwa kumchagua kuwa miongoni mwa wajumbe 15 wa NEC kutoka Zanzibar na kuwaahidi kwamba
ataendelea kuwa mwanachama, kiongozi na
mzalendo ndani nan je ya Chama.
Hata hivyo amewapongeza viongozi mbali mbali wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na Makamu Mwsenyekiti wa CCM Tanzania
bara, Philipo Mangula kwa kuchaguliwa
kwa kura nyingi waendelee kuzitumikia nafasi zao za uongozi.
Pamoja na hayo aliwakumbusha wanachama wa CCM kwamba wao ndio
waajiri wa viongozi wote walioshika nyadhifa mbali mbali ndani ya chama hicho
hivyo ni lazima wawe mstari wa mbele kulinda misingi,itikadi na thamani ya
kisiasa ili maadui waotumia joho la vyama vya kisiasa kutaka kuindosha CCM
madarakani wasifanikiwe kutekeleza mikakati yao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni