MWENYEKITI wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Magalla John Shibuda akizungumza mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Wazazi uliofanyika leo katika ukumbi wa JK-Dodoma. |
IS-HAKA OMAR, DODOMA.
GWIJI wa siasa za Afrika Mashariki, Magalle John Shibuda
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania amesema endapo
vyama vya upinzani vitaweka kando siasa za mihemuko na badala yake wakamuunga
mkono Dkt. Magufuli Tanzania itaingia katika ramani ya nchi tajiri Duniani.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akichambua hotuba ya
Dkt.Magufuli aliyotoa katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Umoja wa Wazazi unaofanyika Dodoma, amesema CCM imepata
bahati ya kuwa na Rais mwenye upeo wa kusoma alama za nyakati kwa kutekeleza
kwa vitendo mahitaji wa wananchi kisiasa, kijamii na kiuchumi.
Mwanasiasa huyo mkongwe Shibuda, amesema wakati umefika kwa
vyama vya siasa kutoa mchango wake wa kumsaidia Rais wa Jamhuri ya muungano
Dkt. John Pombe Magufuli katika vita ya kupambana na vitendo vya rushwa na
ufisadi ili rasilimali zilizopo ziwanufaishe wananchi wote.
Amesema vita hiyo sio ya Chama cha Mapinduzi pekee bali
inahusu maisha ya kila mtu kwani endapo nchi itadhibiti mianya ya upotevu wa
mapato ya serikali kila mtu atanufaika.
Ameeleza wazi kwamba Dkt. Magufuli na Dk. Shein ni Marais wa
kupigiwa mfano mwema katika nchi za bara la Afrika kwani uongozi wao umeleta
mafanikio kwa wananchi na kurejesha heshima ya nchini iliyopotea kwa miaka
mingi hasa katika mgawanyo wa rasilimali za umma.
“ Upinzania hauna maana ya kuwa ni lazima tupinge, kubeza na
kulaumu kila kitu kinachofanywa na serikali kwa nia njema, bali upinzania wenye
manufaa kwa wananchi ni ule unaoshauri, kukosoa na kuibua kero za wananchi ili
serikali itafute ufumbuzi wa kudumu.
Pia naomba nieleweke vizuri kuwa kuunga mkono mambo mema
yanayotekelezwa na Serikali za CCM sio dhambi, hata wapinzani tunayo fursa hiyo
kwani tunanufaika sote”. Anasema Shibuda na kuongeza kuwa vyama vya siasa viwe
ushirikiano kama wa kuni ziwapo jikoni kwani uwaka kwa pamoja ili kuivisha
chakula.
Shibuda, amesema baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani
nchini wametoka katika misingi halisi ya kuwahudumia wananchi kisiasa na badala
yake wamekuwa mabingwa wa kujenga hoja dhaifu za kuviza mambo mema yanayofanywa
na serikali zote mbili ya Zanzibar
pamoja na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amewashauri viongozi
mbali mbali wa Serikali, CCM na jumuiya zake kuyafanyia kazi maelekezo ya
kuleta maendeleo kwa wananchi ili kujenga taifa lenye nguvu za kiuchumi.
Akijibu hoja ya mwandishi wa Habari hizi, kuhusu kauli mbiu
ya Dkt. Magufuli juu ya Sera ya ukuaji wa uchumi kupitia Viwanda, Mwenyekiti
Shibuda ameeleza kwamba hakuna taifa lolote lilofanikiwa kiuchumi bila kupitia
viwanda hivyo na Tanzania ikipitia njia hiyo itaweza kunufaika.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni