Jumatano, 27 Desemba 2017

MWENYEKITI MPYA WA UVCCM TAIFA KHEIR JAMES- ATANGAZA VITA DHIDI YA WATU WANAOWATUKANA VIONGOZI WA CHAMA NA SERIKALI

MWENYEKITI wa UVCCM Taifa Kheir James akiwahutubia vijana wa UVCCM katika hafla hiyo.


NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.


UMOJA wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi(UVCCM) umetangaza rasmi mapambano  dhidi ya watu wanaokashfu na kuwadhalilisha viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi.

Akizungumza Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa, Kheir James na Mamia ya vijana, viongozi wa Chama na Serikali waliojitokeza kupokea msafara wa viongozi wa Umoja huo huko katika ukumbi wa Gymkhana  Afisi Kuu ya UVCCM Zanzibar.

Amesema kuna baadhi ya watu wachache nchini wamekuwa wakijivisha joho la utukufu kwa kuwatukana na kuwadhalilisha viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar huku wakibeza na kudharau kila jambo jema linalotekelezwa  na serikali  hizo.

Mwenyekiti Kheir amewambia vijana wa UVCCM hasa viongozi kuwa wakati wa kuwavumilia  watu wa aina hiyo umekwisha na badala yake ni kuwachukulia hatua stahiki kupitia vyombo vya kisheria.

“Haiwezekani  viongozi wetu wapendwa wanaokesha wakiangaika kwa ajili ya wananchi wa nchi hii, watukanwe sisi tupo sasa kupitia hadhara hii natamka rasmi kwamba yeyote atakayethubutu tena kutukana basi tutamshughulikia,..haiwezekani…haiwezekani lazima tupambane nao.

Nawaagiza vijana wengangu yeyote atakayewavunjia heshima viongozi wetu na sisi tutavunja heshima yake, kwani viongozi wetu wamedhalilishwa mno na wamekuvumilieni sana..Umoja wa vijana tunasema lazima tuchukue hatua haraka iwezekavyo kwa lengo la kurejesha heshima ya Chama na Serikali.”, asisitiza Mwenyekiti huyo.

Ameeleza kuwa wanapotukanwa viongozi wa CCM vyombo vya ulinzi vinakaa kimya wala hakuna anayekamwatwa kwa uhalifu huo, lakini UVCCM ikijibu shutuma hizo vyombo vya ulinzi wanakuwa wakali huku wakida kuwa vijana wanahatarisha usalama wa nchi.

 Akizungumzia lengo la ziara hiyo ambayo ni ya kwanza kufika visiwani Zanzibar  toka uongozi huo uchaguliwe kupitia Mkutano Mkuu wa Tisa wa UVCCM uliofanyika Mjini Dodoma wiki kadhaa zilizopita, amesema lengo ni kuwashukru vijana wote wa UVCCM walioshiriki kwa njia moja ama nyingine kufanikisha uchaguzi uliowapa ridhaa ya kidemokrasia viongozi hao kuchaguliwa ili waongoze jumuiya hiyo kwa miaka mitano ijayo.

Amewasihi viongozi na wanachama wa UVCCM kushirikiana na uongozi huo ili waweze kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa kwa vijana wakati wa kampeni za uchaguzi wa Umoja huo.

Amesema katika uongozi wake atahakikisha anakuwa ni kiongozi wa kusikiliza,kusimamia na kutafuta ufumbuzi wa kero zinazowakabili vijana na sio kutengeneza migogoro na makundi ya kuhatarisha umoja na mshikamano ndani ya UVCCM.

Amesisitiza umuhimu wa vijana wa Zanzibar kushikamana na kupendana ili waweze kunufaika na fursa mbali mbali zinazotokea ndani na nje ya umoja huo kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni