MAKAMU
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Tabia Maulid Mwita
ameishauri serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuongeza kasi katika usimamizi wa mamlaka
zinazohusika na uendeshaji wa kesi za udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake,
watoto na watu wenye ulemavu kuhakikisha zinatenda haki.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati akizungumza katika kipindi
Maalum kinachorushwa mubashara kila siku asubuhi na ridhaa ya Taifa ya Zanzibar
ambayo ni Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC Radio) katika jengo la Shirika
hilo lililopo Rahaleo Mjini Unguja.
Amesema miongoni mwa mikakati ya UVCCM ni kukemea vitendo vya
udhalilishaji wa kijinsia, dawa za kulevya pamoja na vitendo viovu vinavyosababisha
mmomonyoko wa maadili kwa vijana.
Tabia ameeleza kuwa Umoja huo umejipanga kufanya kazi kwa
bidii kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya taasisi hiyo kisiasa na kiuchumi.
Amesema wakati wa vijana kutumiwa kama ngazi ya kufikia
mafanikio kwa baadhi ya watu umekwisha na badala yake vijana hao watumie fursa
zilizowazunguka kujitafutia kipato.
“ Vijana tunatumiwa na baadhi ya wanasiasa hasa inapokaribia
kipindi cha kampeni za uchaguzi na wanapopata nafasi hawaanzishi miradi ya
maendeleo ya kulisaidia kundi hilo ambalo wengi wao hawana ajira za uhakika.
Sasa ifikie wakati na sisi tuwe na misimamo kwa kujiajiri
wenyewe kupitia sekta ya ujasiria mali na ufundi na watushauri mambo mbali
mbali ya kuimarisha taasisi yetu kisiasa.
Kupitia kipindi hicho Makamu Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa
vijana wote nchini kuwaunga mkono viongozi wa Chama na Serikali hasa Mwenyekiti
wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.
Ali Mohamed Shein kwani viongozi wanaojali maslahi ya vijana.
Amesisitiza wananchi kuheshimu utawala wa kisheria kwa
kuepuka uvunjaji wa sheria na miongozo mbali mbali ya nchi.
Pamoja na hayo amewataka viongozi wa UVCCM kuwa mfano wa
kuigwa kivitendo, kauli, maadili, hekima na busara ili vijana wengine waliopo
katika vyama vya upinzani wavutike na kujiunga na umoja huo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni